Main Menu

Friday, December 6, 2013

TANZANIA KUOMBOLEZA MSIBA WA MANDELA KWA BENDERA KUPEPEA NUSU MLINGOTI KWA SIKU TATU

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela

Tanzania imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia tarehe 6 hadi 8 Desemba, 2013, kufuatia kifo cha rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Rais Jakaya Kikwete  ameagiza kuwa katika kipindi hicho cha siku tatu bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Kufuatia kifo hicho Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na kupitia kwake kwa mkewe Bi Graca Machel, wanafamilia wote na wananchi wote wa Afrika ya Kusini kufuatia kifo cha Mzee Nelson Mandela kilichotokea tarehe 5 Desemba, 2013 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Rais kikwete ameuelezea msiba huu kuwa ni msiba mkubwa kwetu sote. 


"Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla imepoteza mtu mashuhuri na shujaa mkubwa wa Karne ya 20 na 21.Tunaelewa machungu waliyonayo wananchi wa Afrika ya Kusini kwa kupoteza kiongozi shupavu, jasiri, mwana mapinduzi , mvumilivu na mstahimilivu". Ameongeza Rais Kikwete.

Rais amemuelezea Mzee Mandela kuwa ni kielelezo cha aina yake kwa wanadamu kwa moyo wake wa kusamehe, huruma na upendo uliomwezesha kuwaunganisha wananchi wa Afrika ya Kusini kuwa taifa moja baada ya kipindi kirefu cha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

"Mandela ni mfano bora kwa wanadamu wa jinsi binadamu muungwana anavyopaswa kuwa . Ni wajibu wa wana Afrika Kusini, Afrika na dunia kuiga mfano wake hasa moyo wake wa uzalendo, kujitolea hata maisha yake kwa ajili yake na wananchi wenzake". Rais ameongeza kusema, "Tuzidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mzee Mandela mahali pema peponi".

Mandela amefariki huko Johannesburg akiwa na umri wa miaka 95 na yeye ndiye aliyeiongoza Afrika Kusini kutoka mikononi mwa watawala wa ubaguzi wa rangi baada ya kufungwa jela kwa miaka 27.

Mandela alikuwa anatibiwa homa ya mapafu nyumbani kwake baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi mitatu.

Katika taarifa yake kwa watu wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, alisema kuwa Mandela amewaaga lakini yuko mahali salama.

Rais Zuma amesema kuwa taifa limepoteza mtu waliyemjua kama mtoto wa taifa hilo.

Mandela aliwahi kushinda tuzo ya amani ya Nobel, na kutambulika kama rais aliyeheshimika sana hasa kwa kupatanisha watu wa Afrika Kusini baada ya kutoka gerezani.

0 comments:

Post a Comment