Main Menu

Sunday, December 8, 2013

JK ATOA CHANGAMOTO KWA UONGOZI MPYA TFF

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametoa changamoto kwa uongozi mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kusukuma mbele zaidi gurudumu la maendeleo ya mchezo huo nchini.

Ametoa changamoto hiyo katika barua yake kwa Rais mstaafu wa TFF, Leodegar Tenga na kumtaka asichoke kutoa ushauri na uzoefu wake kila utakapohitajika katika shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.

Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati akijibu barua ya Tenga iliyokuwa ikimuarifu kuhusu kumaliza kipindi chao cha uongozi, na kumshukuru yeye binafsi (Rais Kikwete) na Serikali anayoiongoza kwa mchango waliotoa katika kuendeleza mpira wa miguu nchini.

“Pongezi zako zimetupa moyo na ari ya kuongeza maradufu juhudi zetu za kuboresha kiwango cha ubora wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.

“Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwako wewe na uongozi wote uliopita wa TFF kwa mchango wenu muhimu mlioutoa wa kuendeleza mpira wa miguu nchini.

“Mafanikio ya kutia moyo yamepatikana chini ya uongozi wako,” amesema Rais Kikwete katika barua yake hiyo na kumtakia kila la heri Tenga katika shughuli zake.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Tanzania bado haijafika pale ambapo inapataka, lakini dalili njema zimeanza kuonekana, hivyo kinachotakiwa sasa ni uongozi mpya kusukuma mbele zaidi gurudumu la kuendeleza mpira wa miguu nchini.

Tenga ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia Desemba 2004 hadi Oktoba 2013.

PAMBANO LA TANZANITE LAINGIZA MIL 5/-
Pambano kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Afrika Kusini (Basetsana) lililochezwa jana (Desemba 7 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 5,353,000.

Washabiki waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika iliyomalizika kwa The Tanzanite kulala mabao 4-1 walikuwa 4,282. Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 816,559.32, gharama za kuchapa tiketi sh. 1,649,754, asilimia 20 ya gharama za mchezo sh. 577,573) wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 433,003.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata sh. 144,334.33 huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh. 1,732,012.01.

Mechi iliyopita ya Tanzanite dhidi ya Msumbiji iliyochezwa Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, na timu hiyo kushinda mabao 10-0 ilishuhudiwa na watazamaji 5,003 na kuingiza sh. 6,190,000.

Tanzanite na Basetsana zitarudiana kati ya Desemba 20 na 22 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.

MECHI YA KILIMANJARO STARS KUPIGWA MACHAKOS
Mechi ya kwanza ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji kati ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na wenyeji Kenya (Harambee Stars) itapigwa Uwanja wa Machakos.

Kwa mujibu wa ofisa wa CECAFA, Amir Hassan mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Machakos ulioko takribani kilometa 64 kutoka jijini Nairobi. Mechi hiyo itachezwa Jumanne (Desemba 10 mwaka huu) kuanzia saa 10 kamili jioni na itaoneshwa moja kwa moja  na kituo cha televisheni cha SuperSport kupitia chaneli ya SS9.

Kilimanjaro Stars imetinga hatua hiyo baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa mikwaju 3-2 ya penalti katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo iliyochezwa jana Uwanja wa Aga Khan katika Jiji la Mombasa.

Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Mabao ya Kilimanjaro Stars yalifungwa na Mrisho Ngasa wakati katika mikwaju ya penalti walofumania nyavu ni Amri Kiemba, Athuman Idd na nahodha Kelvin Yondani.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment