Meneja Rasilimali watu kutoka Shirika la Ndege la Tanzania
(ATCL), Eliezer Mwasele, akishuka kutoka ndani ya ndege mara baada ya ndege ya
Air Tanzania kutua wakati wa uzinduzi wa safari za kwenda Bujumbura- Burundi.
Nyuma yake ni aliekuwa Balozi wa Tanzania Burundi, Francis Mndolwa.
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk. James Nzagi (kushoto)
akiwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Francis Mndolwa (wa pili
kushoto) mara baada ya kupokea ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, Air
Tanzania, iliyoanza sarai za kwenda Bujumbura mwishoni mwa wiki. Wengine mbele
ni baadhi ya mawaziri wa serikali ya Burundi.
Baadhi ya abiria wakipanda ndege ya Shirika la Ndege la
Tanzania –Air Tanzania- kabla ya kuanza safari ya kuelekea Bujumbura –Burundi,
wakati wa uzinduzi wa safari hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya viongozi wakisindikiza abiria walioshuka kwenye
ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania –Air Tanzania- mara baada ya kuwasili
katika uwanja wa ndege wa Bujumbura- Burundi kama ishara ya uzinduzi rasmi wa
safari hizo. Kutoka kushoto ni Waziri wa Burundi wa Afrika Mashariki, Bi
Nziyemana Leontine akifuatiwa na Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dk. James
Nzagi na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Francis Mndolwa
======== ======== ==========
Air Tanzania
yarudisha safari za ndege za kwenda Burundi
· Waanza safari za kwenda Mbeya
· Warejesha safari za Mwanza
SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) limezindua rasmi huduma
za usafiri wa anga kutoka Dar es Salaam kuelekea Bujumbura, Burundi kwa kupitia
mkoani Kigoma, safari hizo zitafanyika mara tatu kwa wiki yaani Jumatano,
Ijumaa na Jumapili.
Hatua hiyo imekuja baada ya hali ya amani kutengamaa katika
nchi hiyo ya Burundi ambayo ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na
kuilazimu Tanzania kusitisha huduma hizo kwa muda wa miaka 20.
Wakati huo huo, ATCL pia imeanza safari za Dar es Salaam
kwenda Mbeya, safari hizo zitafanyika mara nne kwa wiki yaani Jumatatu,
Jumatano, Ijumaa na Jumapili. imerejesha safari za Dar es Salaam – Mwanza kila
siku, safari zilizoanza rasmi Jumapili
iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Bujumbura Burundi
katika uzinduzi wa huduma hizo juzi, Meneja Rasilimali watu wa Shirika hilo la
ndege, Ndugu Eliezer Mwasele, alisema uzinduzi wa safari hizo utakuwa ni njia
mojawapo ya kuchochea maendeleo ya uchumi kwa nchi zote mbili.
Alisema kutokana na hali hiyo Watanzania wanatakiwa
kuchangamkia fursa zilizopo katika nchi hiyo ya Burundi, kwani asilimia kubwa
ya wafanyabiashara wa nchi za Kongo na Burundi wanatarajiwa kuanza kutumia
usafiri huo kwa wingi.
Akizungumzia hatua hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Burundi,
Dk. James Nzagi, alisema kuanza kwa safari hizo ilikuwa ni ndoto ya siku nyingi
ambayo aliipigania na kutamani kuona wananchi wa pande zote mbili wananufaika
kwa pamoja.
“Tumefurahi sana kwa kutimiza ndoto hii leo (juzi), kwa
sababu sasa uhusiano kati ya nchi hizi mbili unazidi kuimarika hasa ukizingatia
tunategemena kibiashara kulingana na fursa zilizopo.
Kwa upande wake, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini
Burundi, Francis Mndolwa, alisema kwa kuwa ATCL imefunga mkanda na kuanzisha
tena safari hizo, ni vyema ikazingatia muda na kuhakikisha huduma stahiki
zinatolewa ili kukuza shirika hilo.
Naye Waziri wa Burundi katika Bunge la Afrika Mashariki,
Nziyemana Leontine alisema, “kuanzishwa kwa Air Tanzania kuja Burundi,
kutasaidia wananchi wa Burundi, hususani wafanyabiashara kwani walikuwa
wanauganisha ndege kupitia nchi nyingine, lakini sasa hivi wananchi watakuja
moja kwa moja. Tunashukuru sana,” alisema.
Naye mmoja wa abiria kutoka Burundi waliopanda ndege hiyo,
Dk. Owera Kodime, alisema, kuanzishwa kwa safari hizo kutawapunguzia sana
gharama za usafiri wananchi wa Burundi, kwa sababu Tanzania imepunguza gharama
kuliko mashirika mengine.
“Tulikuwa tukitumia muda mrefu sana kuzunguka lakini sasa
tutaweza kuja moja kwa moja Dar es Salaam, ni hatua nzuri ambayo imetuletea
faraja sana Warundi,” alisema.
Kwa upande wa abiria kutoka Tanzania, Joseph Kisaro,
alisema, “ Muda mrefu sana kulikuwa hakuna huduma, tangu mwaka 1993 huduma zilikatatika,
lakini uongozi wa Tanzania umefanya juhudi baada ya mapigano kuisha. “Tunashukuru ubalozi ulioteuliwa mwaka 2003 kwani ulianza
harakati haraka za kurudisha huduma hizi ambazo sasa tumefanikiwa.
“Tunaomba uongozi wa ATCL uangalie pia kuwa na safari za
kuelekea Kongo mashariki kwa sababu kuna abiria wengi sana ambao ni
wafanyabiashara wanaokuja Tanzania,” alisema
0 comments:
Post a Comment