Main Menu

Monday, November 25, 2013

SERIKALI ZA MITAA ZISHIRIKIANE NA SEKTA BINAFSI - WAZIRI MKUU,PINDA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema anatamani kuona Serikali za Mitaa hapa nchini zinasimamia maendeleo kuanzia ngazi ya chini kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwa ni njia ya kuharakisha maendeleo kwa wananchi.


Ametoa kauli hiyo huo leo mchana (Jumatatu, Novemba 25, 2013) wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa ushirikiano baina ya Mamlaka za Serikali za Mitaa za China na Tanzania ulioanza leo jijini Dar es Salaam.

“Ni muhimu tukaanzisha ushirikiano huu kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa kwa sababu usimamizi wake unakuwa karibu zaidi na wananchi kuliko ilivyo hivi sasa”, alisema.

Kuhusu ujio wa magavana, mameya na wafanyabiashara wapatao 71 kutoka majimbo manne ya Shandong, Liaoning, Shaanxi na Jilin, Waziri Mkuu alisema ujio wao umekuja wakati muafaka kwani unasaidia kujenga mahusiano ya karibu zaidi na wananchi kwenye ngazi ya chini kuliko inavyokuwa kuna mahusiano kwenye ngazi ya Kitaifa peke yake.

“Hawa waliokuja wanatoka majimbo manne tu kati ya majimbo 31 ya nchi hiyo, tungependa kila mwaka tupate wajumbe wa aina tofauti hadi tufikishe majimbo 15 au 20 hivi... tunataka ushirikiano huu ukue zaidi uende hadi katika miji mikubwa ya Beijing ama Shanghai,” aliongeza.

Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Waziri Mkuu aliwataka watumie fursa hiyo kubadilishana uzoefu na kufanikisha mahusiano ya kibishara si tu baina yao, bali hata katika ngazi ya Halmashauri wanazotoka baadhi ya wajumbe.

Mapema akizungumza na washiriki wa mkutano huo, Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Youqing alisema biashara kati aya China na Tanzania imeongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.47 ambalo ni ongezeko la asilimia 15.2 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka jana.

Alisema hadi kufikia Juni, 2013, makampuni zaidi ya 500 kutoka China yalikuwa yamekwishasajiliwa hapa nchini yakiwa na mtaji wa  Dola za Marekani bilioni 2.175 na kuifanya China iwe ni mwekezaji wa pili kwa ukubwa hapa nchini Tanzania.

Naye Naibu Gavana wa Jimbo la Shandong, Bw. Xia Geng ambaye pia ni kiongozi wa msafara huo, alisema Agosti, 2013 China ilileta madaktari 23 wa fani tofauti ili kusaidia kujenga kada ya watalaam wa sekta ya afya hapa nchini.

Alisema maeneo makuu ambayo wamelenga kuyazingatia katika ziara yao hii ni Kilimo; Nishati; Utunzaji wa Mazingira na uchimbaji wa rasilmali za ardhini.

Alisema ifikapo mwaka 2014, wakati Tanzania na China zinatarajiwa kuadhimisha miaka 50 ya urafiki baina yao, angependa kuona maeneo hayo ya msingi yakiwa yamepewa kipaumbele katika utekelezaji wake.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Asiyekuwa na Wizara Maalum), Prof. Mark Mwandosya, Wakuu wa mikoa 25, Makatibu Tawala wa Mikoa 25, Wakuu wa Wilaya 50, Wakurugenzi wa Halmashauri 95 na wafanyabiashara kadhaa.

0 comments:

Post a Comment