Akizungumza
na Wahariri wa Michezo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Julai 9
mwaka huu), Rais Tenga amewahakikishia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
Dharura kuwa dhamira ya marekebisho hayo ni nzuri, kwani lengo ni kila
mtu apate haki yake.
Amesema
Mkutano huo utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) utakuwa na
ajenda moja tu ya kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya
Maadili katika Katiba ya TFF kama ilivyoelekezwa na FIFA ili baadaye
uanze mchakato wa uchaguzi.
“Katika
kuunda Kamati ya Maadili tumeangalia ile ile ya FIFA, tusitengeneze
kitu kipya, yaondolewe yale yanayotakiwa kuondolewa, na yaongezwe yale
yanayotakiwa kuongozwa. Kwa sababu tumeangalia mazingira kwa Tanzania ni
tofauti na Ujerumani au nchi za sehemu zingine,” amesema.
Rais
Tenga amewataka wajumbe wafike kwenye Mkutano wakiwa na mtazamo wa
kujenga, kwani kuna maagizo ya FIFA ambayo wanatakiwa kuyatekeleza ili
wasonge mbele.
“Tutawaeleza
kwanini hili limewekwa na lile limeondolewa. Mpira unataka unit (kitu
kimoja), ni mchezo wa kila mtu. Baada ya hapa tunaanzisha mchakato wa
uchaguzi. Watu wanaingia wakiwa wamoja, wanatoa hoja wanasikilizwa.
Wanahukumiwa kwa hoja,” amesema na kuongeza utatolewa muda wa kutosha
wajumbe ili wayaone na kuelewa marekebisho hayo.
Rais
Tenga pia alizungumzia kipindi hiki cha usajili na kutaka klabu
ziwaachie wataalamu wa mpira wa miguu kwani ndiyo wanaojua upungufu wa
timu, hivyo wanaweza kusajili wachezaji sahihi.
Amesema
tatizo kubwa la klabu za Tanzania ni kuwa timu zao hazina uwezo wa
kuhimili dakika 90, hivyo watu wanapaswa pia kuzungumzia aina ya mazoezi
ambayo timu zao zinafanya badala ya kubakia kutaja tu majina ya
wachezaji wanaotaka kusajiliwa.
KIINGILIO MECHI YA STARS, UGANDA 5,000/-
Kiingilio
cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa
Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The
Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti
vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000
viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045
kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo
viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio
vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni
sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A
yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Mechi
hiyo ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali
hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika itachezeshwa na mwamuzi
Thierry Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya marudiano itachezwa jijini
Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Tiketi
kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza
kuuzwa siku moja kabla ya mchezo (Ijumaa) katika vituo vifuatavyo; Shule
ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko
mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live
Mbagala na BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi.
Tunapenda
kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika
maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa
fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
MIKOA YATAKIWA KUWASILISHA RATIBA COPA COCA-COLA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linavitaka vyama vya mpira wa miguu
vya mikoa kuwasilisha ratiba zao za michuano ya U15 Copa Coca-Cola kabla
ya Julai 15 mwaka huu.
Ni
vyama vya mpira wa miguu vya mikoa 16 pekee ambavyo ndivyo
vimewasilisha TFF ratiba hizo mpaka sasa. Jumla ya mikoa 32 ya Tanzania
Bara na Zanzibar inashiriki katika michuano hiyo ya umri chini ya miaka
15 kuanzia ngazi ya wilaya ambapo ngazi ya mikoa inatakiwa kuanza Julai
15 mwaka huu.
Mikoa
ambayo tayari imewasilisha ratiba zao ni Arusha, Ilala, Kagera,
Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja, Kigoma, Kinondoni, Kusini Pemba,
Kusini Unguja, Manyara, Mara, Mjini Magharibi, Morogoro, Singida, Tanga
na Temeke.
WASH UNITED YAKABIDHI FULANI 200 KWA KLINIKI YA TFF
Taasisi
ya Wash United inayojishughulisha na usaji na utunzaji mazingira
imeikabidhi fulana 200 na dola 1,000 za Marekani kwa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano
kati yake na TFF yaliyosainiwa Novemba mwaka jana.
Fulana
hizo kwa ajili ya kliniki za kila wikiendi (Jumamosi na Jumapili)
zinazoendeshwa na TFF katika vituo 20 nchini kikiwemo cha Karume ikiwa
ni sehemu ya mpango wa grassroots unaoshirikisha watoto wa umri kati ya 6
na 17 zimekabidhiwa na Mratibu wa Wash United, Femin Mabachi.
Hafla
ya kukabidhi msaada huo imefanyika leo (Julai 9 mwaka huu) kwenye ofisi
za TFF ambapo kwa upande wake ulipokelewa na Ofisa Maendeleo wake Salum
Madadi.
Wash
United inafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la
maendeleo la GIZ, na hapa nchini moja ya eneo wanalotumia katika kampeni
hiyo ili kupambana na magonjwa kama kuhara yanayosababishwa na uchafu
ikiwemo kutonawa mikono vizuri, hivyo kusababisha vifo kwa Watanzania ni
mpira wa miguu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment