Main Menu

Tuesday, July 9, 2013

RAIS WA MPITO WA MISRI ADLY MANSOUR AMETANGAZA RATIBA YA KUFANYIKA KWA UCHAGUZI MPYA

Rais wa mpito wa Misri Adly Mansour ametangaza ratiba ya kufanyika kwa uchaguzi mpya haraka, baada ya mapinduzi ya jeshi dhidi ya rais Muhamad Mursi kusababisha maandamano yaliyogharimu maisha. 


Amri iliyotangazwa na rais huyo inaonyesha kuwa uchaguzi wa bunge utafanyika ndani ya miezi sita, na kufuatiwa na uchaguzi wa rais. 


Lakini tangazo hilo lilikosolewa kwa kurudia makosa ya mpango wa mpito wa mwaka 2011, ambao ulichangia katika mgogoro wa sasa.


Wachambuzi wanasema suluhu ya kisiasa ni muhimu kupatikana haraka iwezekanavyo, baada ya kutokea mauaji ya kutisha dhidi ya waandamanaji wanaopinga kupinduliwa kwa rais Muhamad Mursi siku ya Jumatatu. 


Kundi la Udugu wa Kiislamu, ambalo linaongoza maandamano ya kupinga mapinduzi hayo ya Jumatano wiki iliyopita, lilisema wafuasi wake walichinjwa na wanajeshi na polisi wakati wa sala ya Alfajiri mjini Cairo.


Ujerumani imeelezea kushtushwa na vurugu hizo zilizosababisha vifo vya watu 51, wakati Uturuki imeyaita mauaji hayo shambulio dhidi ya ubinaadamu. 


Qatar, ambayo inaliunga mkono kundi la Udugu wa Kiislamu imetoa wito kwa pande zote kustahamiliana na kuwepo kwa umoja wa kitaifa.

Mauaji hayo yalifanyika wakati rais Mansour alipokuwa anajiandaa kutangaza chaguo lake la waziri mkuu wa mpito.


Chama pekee cha Kiislamu kilichokubali kushiriki katika serikali ya mpito cha Al-Nour kilitangaza kujiondoa baada ya mauaji hayo.

0 comments:

Post a Comment