Kagera
Sugar inaikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo pekee wa Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) utakaofanyika kesho (Mei 11 mwaka huu) kwenye
Uwanja wa Kaitba mjini Bukoba.
Ingawa
timu zote mbili hazipambani kutafuta ubingwa ambao tayari umetwaliwa na
Yanga wala kukwepa kushuka daraja, mechi hiyo bado ni muhimu kwao
katika mazingira matatu tofauti.
Kagera
Sugar inayonolewa na kocha mkongwe kuliko wote katika VPL, Abdallah
Kibaden na ikiwa na pointi 40 yenyewe inasaka moja kati ya nafasi nne za
juu ambazo zina zawadi kutoka mdhamini wa ligi, lakini pia timu
zinazoshika nafasi hizo za juu zinapata tiketi ya kucheza michuano ya
BancABC Super 8.
Kwa
upande wa Ruvu Shooting ya Kocha Charles Boniface Mkwasa yenye pointi
31 inasaka moja ya nafasi sita za juu ambazo ni fursa ya kuingia kwenye
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) ambayo inatarajiwa kuundwa baada
ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Septemba 28 mwaka huu.
Wagombea
nafasi za uenyekiti na makamu wake ni lazima watoke katika timu
zilizoshika nafasi sita la juu katika VPL msimu uliopita. Uchaguzi wa
TPL Board utafanyika siku moja kabla ya ule wa TFF uliopangwa kufanyika
Septemba 29 mwaka huu.
Raundi
ya 25 ya ligi hiyo itakamilika keshokutwa (Mei 12 mwaka huu) kwa mechi
kati ya wenyeji Azam na Mgambo Shooting ya Tanga. Mechi hiyo namba 169
itachezwa katika Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, nje kidogo ya
Jiji la Dar es Salaam.
Azam
yenye pointi 48 inahitaji moja zaidi ili kutetea nafasi yake ya umakamu
bingwa iliyoutwaa msimu wa 2011/2013 na kupata tiketi ya kuiwakilisha
Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Wakati
Azam ikisaka pointi hiyo moja, Mgambo Shooting inayofundishwa na
wachezaji wa zamani wa mabingwa wa Tanzania Bara mwaka 1988, Mohamed
Kampira akisaidiwa na Joseph Lazaro ni moja ya timu ziko katika hatari
ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.
Mgambo
Shooting inahitaji pointi moja tu katika mechi mbili ilizobakiza
kukwepa kurudi FDL, ikishindwa kupata pointi hiyo huku Polisi Morogoro
na Toto Africans ya Mwanza zikishinda mechi zao za mwisho kwa uwiano
mzuri wa mabao itakuwa imekwenda na maji.
Mechi
ya Azam dhidi ya Mgambo Shooting itachezeshwa na refa Jacob Adongo
kutoka Mara, na atasaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Charles
Mbilinyi wa Mwanza. Mwamuzi wa mezani atakuwa Idd Lila wa Dar es Salaam
wakati Kamishna ni Omari Walii wa Arusha.
SIMBA, MGAMBO SHOOTING ZAINGIZA MIL 16
Mechi
namba 149 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Mgambo Shooting
iliyochezwa juzi (Mei 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
na kumalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 imeingiza sh. 16,651,000.
Watazamaji
3,006 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa
sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata
mgawo wa sh. 3,226,125 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
iliyolipwa ni sh. 2,539,983.05.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,640,402.54,
tiketi sh. 3,175,000, gharama za mechi sh. 984,241.53, Kamati ya Ligi
sh. 984,241.53, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
492,120.76 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
382,760.60.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment