Mwandishi wa safu katika magazeti mbalimbali
nchini, Majid Mjengwa amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na
tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF), Absalom Kibanda.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana mchana na
baadaye kuthibitishwa na polisi zinasema Mjengwa alikamatwa muda wa
asubuhi na kwamba alikuwa akihojiwa na makachero wa jeshi hilo hadi
alasiri kuhusu tukio la kuteswa kwa Kibanda.
Msemaji Mkuu wa Polisi Advera Senso aliliambia Mwananchi kwamba:
“Ni kweli kwamba tunaye, tunaendelea kumhoji,
tunachoomba ni kwamba mtupe nafasi ili tufanye kazi yetu na kukiwa na
jambo lolote tutawajulisha.”
Hata hivyo, Senso hakuwa tayari kueleza kwa undani
muda aliokamatwa Mjengwa wala sababu za kukamatwa na kuhojiwa kwake,
lakini chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi kilithibitisha kwamba
pamoja na mambo mengine kuhojiwa kwake kulihusu uteswaji wa Kibanda.
Jumatatu wiki hii, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya
Jinai Nchini, Issaya Mngulu alisikika akizungumza na Kituo cha Radio One
cha Dar es Salaam kwamba kesho Jumatatu (April 15, 2013) polisi watatoa
taarifa rasmi ya hatua waliofikia katika upepelezi wa kesi ya Kibanda.
Kwa upande wake Mia Mjengwa ambaye ni mke wa
Mjengwa, alisema mumewe alipata wito kutoka polisi makao makuu Alhamisi
na kwamba juzi Ijumaa alisafiri kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam
kuitikia wito huo.
“Ninachojua ni kwamba aliitwa kwenda polisi na leo
(jana) alinipigia simu kama saa 7:00 mchana na aliniarifu kwamba yupo
polisi, sasa tangu wakati huo sijaongea naye tena na wala simu zake
hazipatikani,” alisema Mia na kuongeza: “Kwa hiyo mimi kwa kweli
sifahamu kwamba anahojiwa kwa sababu gani.”
Taarifa za kukamatwa kisha kuhojiwa kwa Mjengwa
ambaye pia ni mmiliki wa Mjengwa Blog, zimekuja siku chache tangu
msaidizi wake katika Blog hiyo, Joseph Ludovick akamatwe, kuhojiwa kisha
kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi.
Ludovick alifikishwa mahakamani pamoja na
Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Willifred Lwakatare wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi na kupanga kumteka
Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky.
Kuteswa Kibanda
Machi 5, mwaka huu saa 5.30 usiku, Kibanda ambaye
pia ni Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd,
alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake
kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment