Main Menu

Sunday, April 14, 2013

MBUNGE AOMBA SERIKALI IANZISHE CHUO CHA KUWAFUNDISHA WANAUME KUTONGOZA

MBUNGE wa Viti Maalum, Leticia Nyerere (Chadema), ameitaka Serikali kuanzisha chuo maalumu kwa ajili ya kuwafundisha wanaume jinsi ya kutongoza wanawake.
Akiuliza swali bungeni jana, Nyerere alisema hali hiyo itawezesha wanaume kuachana na ngono ya dezo kwa kuwafuata walemavu wa akili (vichaa), kukidhi mahitaji yao ya kimwili kutokana na kutojitambua kwao.

Alisema kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wanaume kuwapa mimba wanawake wenye ulemavu huo, wakiwamo omba omba na kuwatelekeza.

“Kwa nini Serikali isianzishe kituo cha kuwafundisha wanaume jinsi ya kutongoza wanawake wenye akili zao timamu? Waondokane na ngono ya dezo,” alisema.

Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi na kutaka iwepo adhabu ya kuwahasi wanaume watakaobainika kufanya vitendo hivyo dhidi ya wanawake hao.

Akijibu swali hilo, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani alisema Serikali haiwezi kuanzisha kituo cha aina hiyo na kwamba hiyo ni kinyume cha sheria.

“Zamani mafunzo haya yalikuwa yanafanyika kutokana na mila na desturi za makabila kupitia katika jando.

“Si kwamba wanaume wanaofanya vitendo hivi wanamatatizo, bali ni tabia yao ya kinyama waliyonayo, kufanya mapenzi na kiwete na kumtelekeza ni ukatili mkubwa,” alisema Kombani.

Awali akijibu swali la msingi Kombani alisema, vitendo vya wanaume kuwarubuni wasichana walemavu na kufanya nao ngono ni kinyume cha sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998.

Alisema Serikali imekuwa ikiweka mikakati ya kukabiliana na vitendo hivyo na kwamba sheria hiyo imeweka adhabu ya kifungo cha miaka 30 na faini.

“Sheria inatambua kwamba, wasichana wa namna hiyo hawana uwezo wa kiakili wa kutoa ridhaa ya kujamiiana, hivyo utetezi wa mtuhumiwa kwamba msichana alitoa ridhaa haukubaliki mahakamani.

“Kama msichana aliyedhalilishwa ana umri wa mwaka mmoja au chini ya miaka 10, mhalifu atapewa adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha gerezani,” alisema Kombani.

Aliwataka watu wote wanapoona vitendo hivyo vya kudhalilisha watoe taarifa kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Adhabu zilizoainishwa katika sheria ya kujamiiana ni kubwa na zinatosheleza, hata hivyo kazi ya kutunga na kurekebisha sheria ni kazi ya Bunge.

“Serikali inaridhika kwamba adhabu hii inakidhi viwango vya adhabu iliyopendekezwa katika mikataba ya Haki za Binadamu na katika masharti ya Ibara ya 13 (b) (e) inayozuia adhabu za kutweza,” alisema.

Katika swali lake Nyerere, alitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma na kutaka pia sheria ya kujamiiana irekebishwe, ili kuongeza adhabu kwa watuhumiwa hao.


MTANZANIA

0 comments:

Post a Comment