Main Menu

Tuesday, April 28, 2015

BODI YA LIGI YAENDELEA KUWANYOOSHA WATUKUTU VPL

Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 149 dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga

 Pia Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.

Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa akiba wa timu ya Polisi Morogoro katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu.

Naye Meneja wa Polisi Morogoro, Manfred Luambano alitolewa kwenye benchi la Polisi Morogoro kwa kosa la kutoa lugha za kashfa kwa mwamuzi msaidizi namba moja Martin Mwalyanje. Suala lake linapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Kipa wa Ndanda SC, Wilbert Mweta amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumkanyanga na kutaka kumpiga mwamuzi Eric Onoka kwenye mechi namba 155 dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Kabla ya kufanya kitendo hicho alikuwa ameonyeshwa kadi nyekundu.

Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi na kutaka kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2, Said Mnonga kwenye mechi namba 158 dhidi ya Azam FC iliyochezwa Uwanja wa Azam Compex jijini Dar es Salaam.

Naye Kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuingia kwenye vyumba vya waamuzi na kuwatolea lugha ya matusi mazito ya nguoni baada ya mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5)(c) ya Ligi Kuu.

Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 159 dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Pia Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.

Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mechi (technical meeting) dhidi ya Ruvu Shooting. Mechi hiyo namba 161 ilichezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(2)(a) ya Ligi Kuu.

0 comments:

Post a Comment