KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni,
Freeman Mbowe, amepongeza msimamo wa wabunge hasa wa CCM kwa kuweka
itikadi zao pembeni na kusimamia kidete suala la bajeti ya Wizara ya
Maji, hadi ikasitishwa ili iboreshwe zaidi. Pia kiongozi huyo, pamoja na
kudai kuwa adhabu waliyopewa wabunge watano wa chama chake
haikustahili, lakini akakiri kuwa walihusika katika vurugu ndani ya
Bunge, ikiwa ni pamoja na mmoja wao kudharau mamlaka ya Spika.
Aidha, Mbowe amebainisha kuwa kambi ya
upinzani inataka utaratibu wa mashine za kupigia kura zilizopo ukumbini
kwenye kila meza ya mbunge uanze kutumika mara moja, badala ya kura za
ndiyo na hapana ili kuondokana na mikanganyiko na kutotendeka kwa haki
wakati wa kupiga kura hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini dodoma, Mbowe alisema mshikamano uliojionesha wa wabunge bila kujali
itikadi zao za vyama wakati wa kujadili bajeti ya maji umeonesha
ukomavu wa kisiasa, hali ambayo ndiyo inapaswa iendelezwe bungeni.
“Nashukuru jana (juzi) bungeni wabunge
wengi wakiwamo wa CCM walikataa kuiunga mkono hoja hii ya bajeti kwa
msingi mmoja, kwamba haikidhi mahitaji, na sisi wapinzani kwa kweli hoja
zetu zilipata nguvu kwa sababu takribani wabunge wote walituunga
mkono,” alisema.
Alisema endapo kila siku hali ya
uchangiaji na misimamo ya maslahi ya Taifa itafanyika kama ilivyofanyika
katika hoja ya maji, ni wazi kuwa ushirikiano wa aina hiyo utaijenga
nchi kwa misingi ya maendeleo.
Hata hivyo, Mbowe alitaka Wizara ya
Maji, keshokutwa itakapowasilisha maboresho hayo katika bajeti yake, ije
na mipango thabiti ya kumaliza tatizo la maji nchini, ikiwa ni pamoja
na kuachana na kutafuta Sh bilioni 100 za kuongezewa katika bajeti hiyo
na kutafuta zaidi ya Sh bilioni 500 ili kutekeleza Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Mitano.
Kuhusu adhabu za wabunge watano wa chama
chake kupewa adhabu kwa utovu wa nidhamu, alikiri kuwa mmoja wa wabunge
wa chama chake, alidharau mamlaka ya Spika lakini kanuni zilizotumika
hazikustahili na zilikuwa kiini macho.
Alisema Naibu Spika, Job Ndugai,
hakustahili kutumia kanuni hizo za kifungu cha 2.2 na 5 za Bunge toleo
la mwaka 2013, ambazo zinamtaka Spika atoe uamuzi kuhusu jambo
litakalotokea bungeni endapo katika kanuni zilizopo hazina Mwongozo.
“Ukweli ni kwamba vurugu zilizotokea
bungeni na kitendo cha mbunge wetu Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Tundu
Lissu kinachodaiwa kuwa amedharau mamlaka ya kiti, kanuni zake zipo
pamoja na adhabu yake,” alisema.
Alisema katika kanuni hizo za Bunge,
vifungu 74 na 76 zimebainisha wazi adhabu zinazotakiwa kutolewa kwa
mbunge atakayebainika kudharau mamlaka ya Spika au kuwa chanzo cha
vurugu ndani ya Bunge.
“Ni kweli hakuna shaka kabisa mbunge
wetu alidharau mamlaka ya Spika, lakini zipo adhabu stahiki za
kushughulikia suala hilo, na kwa namna kanuni hizo zilivyo kama
zingetumika vizuri, huenda adhabu ingekuwa kubwa zaidi ya hii
iliyotolewa, huku akiongeza kuwa wabunge hao walioadhibiwa hawakupewa
haki ya kusikilizwa,” alisisitiza.
Adhabu hizo ni pamoja na Spika kutaja
jina la Mbunge husika hadharani kuwa amedharau kiti na kumpeleka mbele
ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka na Bunge na kwa upande wa fujo
zinapotokea ndani ya ukumbi huo wa Bunge, kabla ya kutoa hoja ya nguvu,
hutakiwa kwanza kuahirisha Bunge.
“Siku ile kweli vurugu zilitokea na
kulikuwepo na vitendo vya kudharau mamlaka ya Spika, lakini Naibu Spika
alitakiwa kwanza aahirishe Bunge, ndipo atumie nguvu, sasa badala yake
waliingia askari wa kila aina ndani ya ukumbi jambo ambalo ni kinyume na
Kanuni za Bunge,” alisisitiza.
Aidha, alisema kuhusu suala la adhabu
kwa mbunge anayedharau kiti au kuhusika na vurugu, hutakiwa kwanza Spika
amfikishe mbunge husika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka
ambayo baada ya kushauriana ndipo hutoa adhabu ambayo ni kutohudhuria
Bunge vikao 10 iwapo kosa ni la kwanza na vikao 20 iwapo kosa ni la
pili.
“Adhabu yoyote inayotolewa bungeni
hutolewa kwanza na Azimio la Bunge na si Spika mwenyewe, endapo kanuni
zilizopo zingefuatwa, huenda wahusika kama wangethibitika kabisa kuwa
wamekosa, wangepata adhabu kali zaidi kama zilivyoainishwa kwenye
kanuni,” alisema Mbowe.
Wabunge wa Chadema walioadhibiwa
kutokana na vurugu zilizotokea bungeni humo hivi karibuni pamoja na
Lissu, ni Ezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph
Mbilinyi (Mbeya Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Peter Msigwa
(Iringa Mjini).
Akizungumzia suala la mashine za kura
bungeni, alisema utaratibu unaotumika sasa wa kura za ndiyo na hapana ni
wa zamani na hautendi haki, kwani huegemea zaidi katika uamuzi wa Spika
na si wabunge.
“Lakini Bunge letu lina vifaa
vinavyoonesha namna ya kupiga kura na kuonekana kwenye meza ya Spika,
tena yapo maelekezo yanayomwezesha mbunge husika jina lake lionekane au
la, sasa sielewi kwa nini bado tunang’ang’ania mfumo wa ndiyo na hapana,
hapa kuna mchezo mchafu,” alisisitiza.
Alisema mfumo huo ukitumika, utaongeza
uhuru wa wabunge kupiga kura bila kujali itikadi za vyama na kutanguliza
maendeleo ya wananchi, kwani kwa sasa mtindo wa kura za ndiyo na hapana
hufanya wabunge wengine washindwe kutoa uamuzi sahihi kwa hofu ya
kuitwa wasaliti.
Pamoja na hayo, Mbowe alisema kambi ya
upinzani inaitaka Serikali iwasilishe utekelezaji wa maazimio kuhusu
suala la Richmond, ripoti ya Jairo, maazimio ya kamati ndogo ya
Maliasili na Utalii kuhusu usafirishaji wa twiga na wanyama wengine hai
na suala la mabilioni ya Uswisi.
habari leo chanzo
0 comments:
Post a Comment