Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe jana ameanika majina ya watu saba waliohusika kupitisha mabegi tisa yaliyokuwa na kilo 180 za dawa za kulevya zenye thamani ya Sh8 bilioni, Julai 5 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakiwamo maofisa usalama wanne wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na polisi mmoja.
Alisema mizigo ikishaondoka mikononi mwa abiria
hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa wa Idara ya Usalama wa Taifa, lakini
siku ya tukio hilo mbwa hao walichelewa na walitumika baada ya mizigo
kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.
“Kwa abiria watatu kuwa na mabegi makubwa tisa
yanayofanana si kitu cha kawaida kukwepa jicho la maofisa wa ushuru wa
forodha na vyombo vya usalama, sijui walikuwa wapi siku hiyo?” alihoji
Mwakyembe.
Juzi waziri huyo aliahidi kuyaweka hadharani
majina ya watu wanaosafirisha dawa za kulevya nchini, na alitekeleza
ahadi hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, kusema kuwa
watu hao wamenaswa baada ya mfumo wa kamera (CCTV) za uwanja huo kudaka
matukio kadhaa yaliyotokea siku ya tukio hilo, kuanzia saa 9:25 hadi saa
10:30 alfajiri.
Ameagiza wafanyakazi hao wanne pamoja na askari
polisi mwenye cheo cha koplo, mbeba mizigo na mfanyabiashara aliyekuwa
na wasichana wawili waliokamatwa Afrika Kusini, (ambao hatuwezi kuwataja
kutokana na kushindwa kuwapata kujieleza) kuchukuliwa hatua za
kinidhamu, kukamatwa na kuunganishwa na watuhumiwa waliokwenda na mzigo
huo Afrika Kusini.
Mabegi hayo yaliyokuwa na dawa za kulevya aina ya
‘Crystal Methamphetamine’, yalipitishwa na wasichana wawili wasanii
aliowataja kuwa ni Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward ambao
walidakwa siku hiyohiyo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Afrika
Kusini na tayari wameshafikishwa mahakamani.
Juzi Dk Mwakyembe alifanya ziara JNIA kukagua
utendaji kazi kwenye uwanja huo ikiwa ni siku tatu baada ya ahadi
aliyotoa akiwa Mwanza kwamba katika kipindi cha wiki mbili, atahakikisha
anawakamata vigogo wote walio katika mtandao wa usafirishaji na
uingizaji wa dawa za kulevya kupitia viwanja vyote vya ndege nchini.
Saa nane baada ya ziara hiyo, Maofisa wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege wanadaiwa kumkamata Edwin Monyo akiwa na kete 86 za
dawa aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi aliyokuwa akiisafirisha
kwenda Italia kupitia Zurich.
Mpango ulivyosukwa
Alisema siku ya tukio saa 9:28 kamera hizo za
usalama zilimwonyesha mbeba mizigo wa uwanja huo akiwa anazungukazunguka
eneo la kuingilia abiria kama mtu ambaye ana ahadi na kukutana na mtu
fulani.
“Kamera pia zilimnasa ofisa mwingine wa TAA kwa
mara kadhaa akitoka na kuingia ndani ya jengo la abiria huku akizungumza
na simu, kitendo ambacho hakiruhusiwi kabisa kwa wafanyakazi wa eneo la
ukaguzi wa abiria,” alisema na kuongeza;
“Wakati huohuo, kamera zilikuwa zinamwonyesha
askari polisi anayetuhumiwa kuhusika katika mpango huo akiwa
anarandaranda eneo la uhakiki wa hati za kusafiria kama vile anasubiri
kitu fulani.”
Alisema ilipofika saa 10:15 walionekana Agnes na Melisa wakiwa
na mfanyabiashara huyo katika eneo la kuingilia abiria huku wakiwa na
mizigo na mabegi tisa yaliyofanana.
Alisema kuwa kamera zilimwonyesha polisi huyo
akihangaika kuwasaidia abiria mbalimbali kuweka mizigo yao kwenye
mashine ya ukaguzi, kazi ambayo alieleza kuwa haikuwa yake.
“Mbeba mizigo anayetuhumiwa kuwa katika mtandao
huo alionekana akiwasaidia vijana hao watatu (Agnes, Melisa na
mfanyabiashara) kupeleka mizigo yao kwenye mashine ya ukaguzi na baadaye
kuyazungushia mabegi hayo katarasi za nailoni na kuyafikisha kaunta ya
Shirika la Ndege la Afrika Kusini,” alisema.
Alisema kamera hizo zilimnasa ofisa wa TAA
akimwondoa katika kiti cha ukaguzi wa mizigo mfanyakazi mwenzake, na
kukaa yeye ikiwa ni dakika chache kabla ya mabegi tisa ya vijana hao
hayajaingia katika mashine ya ukaguzi.
“Kinyume na taratibu ofisa huyo hakujiandikisha
kwenye kitabu cha wakaguzi (Screener’s logbook), saa 10:16 akaanza
kupitisha mabegi hayo tisa mpaka saa 10:22. Alipomaliza kupitisha mizigo
hiyo kwa dakika sita akamwachia ofisa aliyekuwa katika eneo hilo na
kuondoka,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema ofisa huyo baada ya kuondoka katika kiti
hicho alizungumza kwa dakika kadhaa na askari polisi anayedaiwa kuwa
katika mtandao huo na kurejea tena sehemu aliyokaa ofisa mwenzake wa TAA
na kumnong’oneza jambo fulani.
“Baada ya hapo akaelekea ukumbi wa abiria huku
akiongea na simu, mambo hayo yote yalifanyika huku kiongozi wa sehemu ya
ukaguzi akiwa hapohapo bila kushtuka,” alisisitiza.
Alisema baada ya mizigo hiyo kupita katika mashine
ya ukaguzi (baggage screening machine), vijana wale watatu wakahamia na
mizigo yao kwenye kaunta ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.
“Mabegi matatu ya kilo 20 kila moja yalipitishwa
yakabaki mabegi sita ambayo yalitakiwa yalipiwe malipo ya uzito wa
ziada.
Kwa taratibu za shirika hilo kila kilo moja inayoongezeka hulipiwa dola 5 (Sh8,000), vijana wale walitakiwa kulipia dola 600, lakini walitozwa dola 94 tu ambazo zinathibitishwa na risiti tuliyonayo,” alisema.
Kwa taratibu za shirika hilo kila kilo moja inayoongezeka hulipiwa dola 5 (Sh8,000), vijana wale walitakiwa kulipia dola 600, lakini walitozwa dola 94 tu ambazo zinathibitishwa na risiti tuliyonayo,” alisema.
Alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida
mfanyabiashara ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiri siku hiyo, baadaye
alibadili mawazo hapohapo na kuamua kuondoka siku hiyo kwenda Afrika
Kusini na kulipia gharama ya dola 60 (Sh96,000) ili kupata tiketi.
“Kutokana na hali hiyo mhakiki wa nyaraka za
safari nje ya ukumbi wa abiria siku hiyo, hakupaswa kumruhusu
mfanyabiashara kuingia ndani ya ukumbi bila tiketi ya siku hiyo,”
alisema na kuongeza;
“Kwa hali ya kawaida mizigo ikishaondoka mikononi
mwa abiria hukaguliwa tena kwa kutumia mbwa, lakini siku hiyo mbwa
walichelewa na walikuja kutumika baadaye ikiwa ni baada ya mizigo
kuingizwa kwenye masanduku ya chuma.”
Hatua za wizara
Alisema wizara imeagiza TAA kuwa, kuanzia sasa mtu
yeyote anayekamatwa na dawa za kulevya lazima apigwe picha na
zisambazwe kwenye vyombo vya habari.
Pia ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na
Polisi wa Kimataifa (Interpol) kumkamata mfanyabiashara anayedaiwa
kuwasaidia Masogange na mwenzake kusafirisha dawa za kulevya ambaye
alitoweka na mabegi matatu ya dawa hizo huko Afrika Kusini, “Akamatwe na
kuunganishwa na kesi inayowakabili Watanzania hao wawili.”
Alisema mbeba mizigo anatakiwa kufukuzwa kazi na
mwajiri wake na asiruhusiwe kukanyaga JNIA, kwamba serikali imewaagiza
polisi kumkamata mtu huyo kwa lengo la kuunganishwa na wenzake kujibu
mashtaka ya jinai chini ya sheria ya kuzuia dawa za kulevya, sura ya 95
ya mwaka 1996.
Alisema TAA inatakiwa kuwafukuza kazi mara moja
wafanyakazi wake wanne waliohusika katika mpango huo, kuwakamata na
kuwaunganisha katika mashtaka yanayowakabili.
“Jeshi la polisi limeagizwa kumwondoa mara moja
askari mwenye cheo cha koplo anayedaiwa kuhusika katika tukio hilo na
kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kushiriki kwake kwa njia moja au
nyingine kwenye njama za kupitisha mabegi hayo ya dawa za kulevya,”
alisema.
Alifafanua kuwa Idara ya Usalama wa Taifa
imeagizwa kuendesha uchunguzi wa kina kwa maofisa wake waliokuwa zamu
siku ya tukio kwa kuchelewa kuwafikisha mbwa wakati mwafaka, jambo
ambalo limeliletea taifa fedheha kubwa.
“Serikali imeziagiza taasisi zote zilizopo chini
ya JNIA kutekeleza majukumu ipasavyo na kwa mujibu wa sheria na taratibu
ili kuhakikisha dawa za kulevya hazipiti kwenye kiwanja hicho kikuu cha
ndege nchini,” alisisitiza.
NA gazeti mwananchi
NA gazeti mwananchi
0 comments:
Post a Comment