Hivi karibuni kulitolewa taarifa katika chombo kimoja cha habari kikidai kwamba wapo watumishi wa Wizara ya Ujenzi wanaolalamikia ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma katika zabuni hiyo.
Mwandishi wa gazeti hilo ambaye amejitambulisha kama ‘Mwandishi Wetu’ ameendelea kuandika kuwa wapo pia baadhi ya wafanyakazi wa TEMESA wanaodai kuwepo kwa usiri katika manunuzi ya mashine hizo za kukatia tiketi. Aidha, kwa eneo lingine la taarifa hiyo mwandishi anadai kwamba malalamiko yametoka kwa wadau/mdau.
TEMESA inapenda kutoa taarifa rasmi kwamba taratibu zote za manunuzi ya mashine hizo zilizingatiwa kwa kutumia Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004 na kanuni zake za 2005. Suala la usiri halikuwepo katika zabuni hii kwa kuwa utaratibu wote wa zabuni uliendeshwa na kusimamiwa na Kamati ya Manunuzi pamoja na Bodi ya Manunuzi ya Wakala, vyombo ambavyo vimewekwa kwa misingi ya sheria ya manunuzi. Sheria hiyo pia inaelekeza taratibu za rufaa kwa mzabuni ambaye hajaridhika na tathmini ya zabuni husika.
Aidha, manunuzi yote kuhusu vivuko vya Serikali na huduma zake hapa nchini yanafanywa na TEMESA kupitia Bodi yake ya Zabuni. Wizara kama msimamizi wa Wakala huu hupokea taarifa za utekelezaji. Hivyo, TEMESA ndiyo mamlaka iliyoshughulikia ununuzi wa mashine hizo.
Kwa mujibu wa mkataba, mzabuni aliyefunga mashine hizo yupo katika kipindi cha uangalizi kwa mwaka mmoja. Katika kipindi hicho jukumu lake ni kuangalia mashine alizozisimika na kutoa mafunzo ya uendeshaji kwa watumishi. Mashine hizo za kukatia tiketi zimeanza kufanyakazi tarehe 21/05/2013. Pamoja na kufungwa mashine za kukatia tiketi pia katika kituo hicho kumefungwa kamera maalum za kufuatilia mwenendo wa ukatishaji tiketi katika eneo hilo.
Tofauti na taarifa ya gazeti hilo kuwa, tangu kufungwa kwa mashine hizo za kukatia tiketi mapato yamekuwa yakishuka kwa kasi, ukweli ni kwamba makusanyo yamekuwa yakiongezeka kwa kiwango cha kuridhisha tangu kufungwa kwa mashine hizo ikilinganishwa na hapo awali. Aidha, TEMESA ndiyo inayokatisha tiketi na kukusanya mapato hayo na wala sio mzabuni anayeifanya kazi hiyo kama mwandishi wa gazeti hilo alivyodai katika taarifa yake.
Kwa kutambua majukumu ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa mujibu wa Sheria za Wakala Namba 30 ya 1997, Wakala unapenda kuarifu kwamba utaendelea kusimamia masuala ya manunuzi yote kwa misingi na taratibu za sheria, na utaendelea kuelekeza nguvu katika kuhakikisha mapato yatokanayo na vivuko yanakusanywa kwa ufanisi. Tayari Wakala umekwishaa anza kutumi portable electronics machines katika vivuko vingine.
Kutokana na mafanikio ya mfumo huu ulioonekana katika Kivuko cha Magogoni, Wakala unakusudia kueneza mfumo huu (electronic ticketing) katika vivuko vingine hapa nchini hatua kwa hatua.
Taarifa hii imetolewa na:
Eng. Marcellin Magesa
MTENDAJI MKUU
0 comments:
Post a Comment