Main Menu

Sunday, June 9, 2013

MASHUJAA BAND, OMMY DIMPOZ, NA KALA JERE100 WAFUNIKA TUZO ZA KILI MUSIC AWARDS 2013



Ulikuwa ni usiku wa Mashujaa Band ambayo ilizoa tuzo tano kwa mpigo katika fainali za Kilimanjaro Music Award zilizofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mashujaa ambao wanatamba na wimbo wao wa Risasi kidole waliweza kunyakua tuzo ya Msanii bora wa kiume wa bendi ambayo ilikwenda kwa Charz Baba pamoja na ile ya Mtunzi bora wa Mashairi ya bendi wakati ya Rapa bora iliyokwenda kwa Furguson.

Tuzo ya nne iliyoibeba bendi hiyo yenye maskani yake Vingunguti na kuwabwaga wapinzani wao ni ile ya Wimbo bora wa bendi kupitia wimbo wao wa Risasi Kidole ambao walichuana na Mapacha Watatu (Chanzo ni Sisi), Shamba la Twanga (African Stars), na Jinamizi la Talaka (Mlimani Park).


Mashujaa walifunga kazi baada ya kutwaa tuzo ya bendi bora ya mwaka ambayo walikuwa wakiwania na Twanga Pepeta, Mapacha Watatu, Msondo Ngoma, na Mlimani Ochrchestra 'Sikinde'.

Akizunguza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Charz Baba alisema aliwashukuru mashabiki kwa kuwapigia kura na kuwawezesha Mashujaa kuibuka kidedea katika fainali hizo huku akichombeza wimbo wa Risasi Kidole, kama kidole kingekuwa risasi basi wao wasingekuwepo.

Msanii mwingine ambaye aling'ara kwenye tuzo hizo ni Kalla Jeremia sambamba na Ommy Dimpoz ambao wote kila mmoja aliondoka na tuzo tatu.

Kalla Jeremiah alinyakua tuzo ya wimbo bora wa mwaka (Dear God), Mtunzi bora wa Mashairi wa Hip Pop na Msanii bora wa Hip Pop, wakati Dimpoz alinyakua ya Video bora ya wimbo wa Mwaka (Badae), wimbo bora wa bongo Pop na wimbo bora wa kushirikiana wa Me and U ambao alimshirikisha Vanesa Mdee huku tuzo kubwa kabisa ya All Fame (Waliochangia mafanikio ya muziki) ilikwenda kwa Kilimanjaro Band 'Wana Njenje' maarufu 'Kinyaunyau'.

Wasanii wengine ambao hawakutoka kapa ni Dimond Platinums 'Sukari ya Warembo' alitwaa tuzo mbili msanii bora wa kiume na ile ya ile ya msanii bora wa kiume bongo fleva, wakati ile ya msanii bora wa kiume wa taarabu ilikwenda kwa Mzee Yusuf, Msanii bora wa kike ilikwenda kwa Lady Jay Dee ambaye hata hivyo hakuwepo na badala yake alipokelewa na mumewe Gadna Habash, na ukumbi ulilipuka kwa vifijo baada ya wimbo wake unaotamba hivi sasa Joto Hasira kurindima.


"Sina mengi ya kusema, nawashukuru watanzania kwa kumpigia kura mke wangu na kufanikiwa kutwaa tuzo hii, Joto Hasira itazinduliwa Juni 14."

Msanii bora wa kike wa bendi imechukuliwa na Luiza Mbutu, tuzo ya anayechipukia imekwenda kwa Ali Nipishe, Mtunzi bora mashairi ya taarabu imechukuliwa na Thabit Abdul, Mtunzi bora mashairi Bongo Fleva ni Ben Poul, huku mtayarishaji bora wa mwaka kizazi kipya ni Man Walter wakati ile ya ile ya mtayarishaji wa wimbo bora taarabu imechukuliwa na Enrico.

Nyingine ni mtayarishaji wimbo bora wa mwaka bendi imechukuliwa na Amarosso, mtayarishaji chipukizi wa mwaka ni Mansen Selecta, vionjo vya Asili imetwaliwa na Mrisho Mpoto, tuzo ya Reggae imekwenda kwa Kilimanjaro Warrious from the East, wakati ile ya Wimbo bora Afrika Mashariki imechukuliwa na Jose Chamelleon.


Tuzo ya wimbo bora wa Hip Pop imekwenda kwa Ney wa Mitego 'Nasema Nao' Ragga/Dancehall imechukuliwa na Predator Dabo, Wimbo bora wa taarabu ni Khadija Kopa, Zhouk/Rhumba imechukuliwa na Amin kupitia wimbo wake wa 'Ni wewe' kikundi bora cha taarabu (Mashauzi Classic) na kikundi bora cha muziki kizazi kipya ni Jambo Squard kutoka Arusha.


0 comments:

Post a Comment