Main Menu

Thursday, March 7, 2013

TUME HURU YA UCHAGUZI NA MIPAKA NCHINI KENYA YAKANUSHA KUCHAKACHUA MATOKEO

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya IEBC  amekanusha madai kwamba tume hiyo imekuwa ikifanya udanganyifu na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi wa rais nchini humo.

Ahmad Isaack Hassan amesema kuwa, zoezi la kuhesabu kura kwa mikono limetekelezwa baada ya kujitokeza hitilafu  ya mitambo ya elekroniki ya kuhesabia kura  nchini humo.

Hadi sasa karibu kura milioni nane zimeshahesabiwa, na  Uhuru Kenyatta mgombea kutoka muungano wa Jubilee anaongoza akifuatiwa na Raila Odinga kutoka muungano wa CORD.

Uchaguzi mkuu nchini Kenya ulifanyika siku ya Jumatatu iliyopita, ambapo imeelezwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watu milioni 14 na laki tatu waliokuwa na sifa ya kupiga kura, walishiriki kwenye uchaguzi huo.


Wakati huohuo, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC iliyoko The Hague nchini Uholanzi  imeakhirisha kusikiliza kesi inayomkabili Uhuru Kenyatta pamoja na baadhi ya wanasiasa wengine wa nchi hiyo.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa mwezi ujao wa Aprili, imeakhirishwa hadi mwezi Julai mwaka huu.

Uhuru Kenyatta pamoja na mgombea mwenza wake William Ruto na wanasiasa wengine wa nchi hiyo wanatuhumiwa kwa vitendo vya ukiukaji wa  haki za binadamu na kutenda jinai dhidi ya binadamu katika matukio yaliyojiri baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 nchini humo.

Imeelezwa kuwa zaidi ya watu 1,100 waliuawa kwenye machafuko hayo.

MWISHO.

0 comments:

Post a Comment