Serikali imeanza kutoa Nishani kwa wasanii kwa vile inatambua umuhimu wao katika jamii.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amewaeleza wawakilishi wa sanaa mbalimbali nchini
waliofika Ikulu leo asubuhi kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa
kuwatambua na kuwapa heshima kubwa ya Tuzo na Nishani wasanii katika
siku ya sherehe za Uhuru za tarehe 9 Disemba, Ikulu, Dar-Es-Salaam.
“Tumetoa
Nishani kwa vile wasanii wanatoa mchango mkubwa, tumeanza kutoa nishani
mwaka huu na tutaendelea kutoa miaka ijayo kwani kwa kuitambua sanaa,
mnawapa moyo wasanii kuendelea kujituma na kuwa wabunifu zaidi” Rais
amesema na kuongeza, “Tumeingiza Nishani ya Wasanii na Watafiti maana
nao wanafanya kazi kubwa sana ya kutafiti mazao na mbegu mbalimbali
ambazo zinaongeza tija katika kilimo nchini”.
Katika
kumbukumbu ya kusherehekea miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania bara mwaka
huu, Rais Kikwete alitunuku nishani kwa makundi mbalimbali ya watu
waliotoa mchango mkubwa katika jamii na waliotumikia taifa kwa uadilifu.
rais kikwete na mwanamuziki hamis mwijuma (binamu)
Rais
alitoa Nishani ya Sanaa na Michezo kwa mara ya kwanza kwa wasanii
nchini ambapo Bi. Fatma Baraka Khamis (Bi Kidude) kupitia Baraza la
Sanaa Zanzibar, Kiongozi wa Muziki wa Dansi ya Msondo Ngoma Muhidin
Maalim Gurumo, Kiongozi wa Zamani wa Bendi ya Dar Intrenational Marehemu
Marijan Rajab walipata tuzo hiyo.
Wengine ni Msanii wa maigizo na filamu nchini Marehemu Fundi Said (Mzee Kipara) na Mwanariadha mkongwe John Steven Akwari.
Rais
amewataka wasanii kushirikiana na serikali lakini pia wawe mstari wa
mbele katika kupigania haki zao na sio kusubiri serikali tu iwafanyie
hivyo.
Wasanii hao wamefika Ikulu wakiongozwa na Bw. Ruge Mutahaba wa Clouds Media Group.
Wengine
ni Addo Mwasongwe, Rais wa Shirikisho la Muziki na Mwenyekiti wa Chama
cha Muziki wa Injili, Bw. Juma Ubao Mwenyekiti wa Chama cha Muziki
Tanzania (CHAMUDATA), aliyewakilishwa na Hamza Kalala.
Bibi
Shakila Said, Mkongwe wa Muziki wa Taarab Nchini, Bi Carola Kinasha
Msanii wa Muziki , Mzee King Kiki msanii wa Muziki wa Dansi Mwana FA,
msanii wa Kizazi Kipya na Bw. Waziri Ally , msanii wa Muziki.
Wawakilishi
hao pia wamemshukuru Rais kwa msaada wa hali na mali anaotoa kwa
wasanii mbalimbali wanapopata matatizo ambao hivi sasa wapo katika hatua
mbalimbali za matibabu ya afya zao hapa nchini na nchi za Nje.
“Haya
mengine ninayafanya tu kama wajibu wa kibinadamu kwa vile nina nafasi
ya kufanya hivyo na pale tunapokua na uwezo tunasaidia kama binadamu
wenzetu” Rais Amesema.
Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu - DSM
21 Desemba, 2012
0 comments:
Post a Comment