
Taifa Stars ambayo
ilikuwa kambini nchini Ethiopia kwa takribani wiki moja, iliondoka jana usiku
Addis Ababa na kuwasili uwanja wa ndege wa Cairo majira ya saa 8 usiku,
kisha kuunganisha kwa usafiri wa basi mpaka Borg El Arab takribani masaa
matatu.
Kocha mkuu wa Taifa
Stars Mart Nooij, atakiongoza kikosi chake katika mazoezi ya mwisho leo saa 1
usiku katika uwanja wa Borg El Arab kwa saa za Misri, sawa na saa 2 usiku kwa
saa za Afrika Mashariki.
Akiongelea mchezo wa
kesho, Nooij amesema anashukuru kikosi kimefika salama nchini Misri na kipo
katika hali nzuri, vijana wana ari na morali ya hali ya juu, anaamini kesho
timu itfanya vizuri katika mchezo huo dhidi ya wenyeji Misri.
Nooij amesema mchezo
wa kesho ni muhimu kwake, na kikosi chake kitacheza mpira wa kasi na pasi za
haraka haraka, huku safu ya ushambuliaji ikihakikisha inatumia vizuri nafasi
itakazozipata.
Aidha kuelekea katika mchezo huo wa kesho,
kiungo Amri Kiemba ameungana na wachezaji wengine waliokuwa kambini Addis Ababa
kuchukua nafasi ya Mrisho Ngasa ambaye alishindwa kuungana na timu kutokana na
sababu zilizopo nje ya uwezo wake.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Juma Nkamia tayari amewasili jijini Alexandria kwa ajili ya kuipa
sapoti Taifa Stars katika mchezo huo wa kesho.
Mchezo kati ya Misri na Tanzania utachezwa
kesho saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na kati katika uwanja wa jeshi la
Misri (Borg El Arab) uliopo takribani kilometa 70 kutoka jijini Alexandria na
kilometa 200 kutoka jiji la Cairo.
0 comments:
Post a Comment