Main Menu

Wednesday, July 3, 2013

TANZANIA YATAKATA KIMATAIFA KWA ZIARA YA OBAMA

Mashirika mbalimbali ya habari duniani yameripoti ziara ya Rais Barrack Obama wa Marekani alipokuwa nchini, kila moja likielezea umuhimu wa ziara hiyo kwa namna yake.

 
Mbali na mashirika hayo makubwa pia vyombo vya habari vya Tanzania havikuwa nyuma katika kuripoti matukio mbalimbali ya ziara hiyo.


Shirika la Habari la Uingereza (BBC), limeielezea ziara hiyo ya Rais Obama kuwa ililenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika, huku kukiwa na wasiwasi kuwa Marekani inaachwa nyuma na China katika uhusiano wao na Afrika.


BBC imeeleza kuwa baadhi ya Watanzania kupitia mitandao ya kijamii wamekosoa ziara ya Obama katika nchi yao, wakisema kuwa ziara yake imeathiri shughuli za maisha ya kila siku.


Shirika la CNN la Marekani, limeelezea ziara hiyo ya Rais Obama kuwa ni kutokana na Tanzania kuwa mshirika muhimu wa usalama na maendeleo ya kiuchumi na kwamba alitaka kuonyesha uwezo wake wa kiuchumi dhidi ya China.


Limeeleza kuwa kutokana na Tanzania kuwa pembeni mwa Pwani ya Bahari ya Hindi na nchi za jirani kukosa bandari, hivyo ni nafasi ya kampuni za Marekani kupanua fursa za kibiashara kupitia bandari za Tanzania.


Kwa upande wa gazeti la Washington Post, lilijikita katika kuelezea ziara hiyo kama ni ya kibiashara na kueleza jinsi Obama na Rais mstaafu wa nchi hiyo, George Bush watakavyokutana Tanzania kuwa ni tukio la kihistoria.


Viongozi hawa walikutana na kuweka shada la maua ikiwa ni kumbukumbu kwa waliokufa katika Ubalozi wa zamani wa Marekani uliolipuliwa kwa bomu mwaka 1998.


Gazeti la New York Times limeeleza ziara hiyo kama ya kukuza ushirikiano kibiashara wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.


Pia gazeti hilo limezungumzia mapokezi ya Obama nchini Tanzania kwamba yalikuwa ni makubwa kuliko aliyoyapata Senegal na Afrika Kusini.


Shirika la Utangazaji la Marekani, Sauti ya Amerika (VOA), limeeleza ziara hiyo ni ya kujadili mipango na hatua za juu za ushiriki wa kiuchumi wa Bara la Afrika na “mtindo mpya” wa misaada ya Marekani katika bara hilo.

chanzo mwananchi.

0 comments:

Post a Comment