Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru washabiki kwa kujitokeza
kwa wingi kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars
na Ivory Coast (The Elephants) iliyochezwa juzi (Jumapili) kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwitikio
wa washabiki katika mechi hiyo ilikuwa ni moja ya chachu ya kiwango
kilichoonyeshwa na Taifa Stars, kwani walishangilia mwanzo hadi mwisho
licha ya kupoteza kwa mabao 4-2.
Ni
matarajio utakuwepo mwitikio kama huo huo katika mechi ijayo ya Taifa
Stars ya michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Nyumbani (CHAN)
dhidi ya Uganda (The Cranes) itakayochezwa Dar es Salaam kati ya Julai
12-14 mwaka huu. Stars itaingia tena kambini Julai 4 mwaka huu kujiandaa
kwa mechi hiyo.
RWIZA KUHUDHURIA SEMINA YA MAKAMISHNA CAF
Kamishna
Alfred Kishongole Rwiza ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) kuhudhuria semina ya makamishna itakayofanyika kuanzia
Julai 6-7 mwaka huu katika makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo,
Misri.
Semina
hiyo inashirikisha baadhi ya makamishna wa CAF walioko kwenye orodha ya
makamishna ya shirikisho hilo kwa mwaka 2012-2014.
Rwiza
ni mmoja wa makamishna wa CAF kutoka Tanzania, na mechi ya mwisho
kusimamia ilikuwa ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Mei mwaka huu
nchini Msumbiji.
CAF tayari imeshamtumia tiketi Rwiza, na anatarajia kuondoka nchini Julai 4 mwaka huu kwenda Cairo kwa ndege ya EgyptAir.
MTANZANIA APEWA ITC ACHEZE YEMEN
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa
(ITC) kwa mchezaji Mtanzania Gossage Mtumwa ili aweze kucheza mpira
nchini Yemen.
Mtumwa
ambaye anatoka katika kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha
Rollingstone cha Arusha aliombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu
cha Yemen (YFA) kwa ajili ya kucheza nchini humo.
TFF
inamtakia kila la kheri Mtumwa katika safari yake ya Yemen, na ni
matarajio yetu kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini humo ili
wachezaji wengine wa Tanzania nao wapate fursa ya kucheza mpira wa miguu
nchini Yemen.
KLABU THAILAND YASAKA WACHEZAJI TANZANIA
Klabu
ya Thai Port Football ya Thailand inatafuta wachezaji nchini Tanzania
kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu nchini humo na katika nchi nyingine
barani Ulaya.
Kupitia
kwa wakala wake, klabu hiyo imetuma taarifa kupitia Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) ikitaka wachezaji wenye umri kuanzia miaka 15
hadi 28 kwa ajili ya kuwafanyia majaribio ambapo watakaofuzu watacheza
nchini humo na katika klabu nyingine za Ulaya ambazo wana ushirikiano
nazo.
Wachezaji
wenye nia ya kufanya majaribio wanatakiwa kutuma taarifa za wasifu wao
(CV) kwa klabu hiyo kwa njia ya emaili, wawe na pasi ya kusafiria pamoja
na pasi ya mchezaji (player passport).
Wakala
atapitia vitu hivyo, na kwa wachezaji atakaowahitaji atawatumia tiketi
za ndege na viza kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio nchini humo, na
watakaofanikiwa kabla ya kusaini nao mikataba watawasiliana na klabu zao
nchini (kwa wale wenye klabu).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment