Main Menu

Monday, March 4, 2013

MUGABE AFANYA KUFURU KWENYE BIRTHDAY YAKE





Bindura, Zimbabwe
Bindura. Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amefanyiwa sherehe ya kufuru nchini humo ambapo imegharimu zaidi ya Dola 600,000.

Habari kutoka Zimbabwe zilisema kwamba pesa hizo zimetolewa na kampuni mbalimbali kwa lengo la kufanikisha sherehe hiyo ya kuzaliwa kwake ambapo anatimiza miaka 89.
Mbali na hayo, lakini watu wenye maduka mjini Bindura walisema waliamrishwa kufunga maduka mapema ili kusaidia kusafisha mji kwa ajili sherehe  ya siku ya kuzaliwa kwa Rais.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo Rais Robert Mugabe alisema kwamba ana matumaini ya kushinda katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo.
Alisema  anaamini atamshinda hasimu wake katika uchaguzi ujao wa rais uliopangwa kufanyika mwaka huu na kubakia madarakani kwa miaka mingine mitano.
Aidha Rais huyo mkongwe  aliwatuhumu wapinzani wake kuwa, wanakusudia kuzusha machafuko ya kisiasa nchini humo kwa lengo la kumfanya ashindwe kwenye uchaguzi ujao.

Kwenye sherehe ya  kwanza iliyofanyika mwezi uliopita, Mugabe alisema jukumu lake la kuongoza Zimbabwe amepewa na Mungu.

Wapinzani wake wana wasiwasi kuwa wafuasi wa Mugabe wanapanga kuanza tena ghasia na vitisho wakati nchi inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.
Walisema tayari ofisi za makundi yanayochunguza uchaguzi zimeshambuliwa na polisi wamenyang'anya watu mamia ya redio za kuweza kusikiliza matangazo ya mbali.
Wakati Rais huyo akifanya sherehe ya gharama kubwa kiasi hicho  Waziri wa Fedha wa Zimbabwe, Tendai Biti alitangaza kwamba Serikali ya nchi hiyo imebakiwa na kiasi cha Dola 217 pekee ambazo ni sawa na Sh343,000 za Tanzania.
Salio hilo liliwastua wengi kwani nchi hiyo yenye utajiri wa kutosha wa madini ya almasi kwa mwaka jana pekee iliweza kukusanya Dola 685 milioni za Marekani.
Biti alisema kwamba pesa hizo zote zilitumika kuwalipa mishahara watumishi wa Serikali.

Kukosekana kwa pesa kunawafanya viongozi wakose amani kwa kuwa mwaka huu wanakabiliwa na Uchaguzi Mkuu.

0 comments:

Post a Comment