Main Menu

Thursday, February 21, 2013

JAJI MKUU WA KENYA ATISHIWA MAISHA

Jaji Mkuu wa Kenya Willy Mutunga amesema kuwa ametishiwa kifo na kutahadharishwa kwamba asithubutu kumzuia Uhuru Kenyatta kugombea katika uchaguzi ujao nchini humo.

Willy Mutunga, amesema maisha yake yamo hatarini baada ya kupokea vitisho kuhusiana na kesi ya maadili inayomkabili mgombea urais wa Muungano wa Jubilee Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza William Ruto.

Hata hivyo, amesema vitisho kama hivyo havitamtetemesha na yuko tayari kufa ilimradi anaitetea katiba ya nchi.

Wiki iliyopita Mahakama Kuu nchini Kenya imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa na makundi ya kijamii kupinga Uhuru Kenyatta na William Ruto kuwania nyadhifa za rais na makamu wake kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Majaji waliokuwa wakishughulikia kesi hiyo wamesema Mahakama ya Kilele pekee ndiyo yenye uwezo wa kisheria wa kusikiza kesi hiyo.

Kenyatta anakabiliwa na kesi ya kimaadili ambapo anatuhumiwa kufadhili kundi la Mungiki fedha ambalo lilifanya mashambulizi mwaka 2007 dhidi ya Waziri Mkuu Raila Odinga alipokuwa kiongozi wa upinzani wakati huo.

Mwanasiasa huyo wa Kenya pia anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.


0 comments:

Post a Comment