MATOKEO ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 yaliyotangazwa mwanzoni mwa
juma, yanaendelea kutawala mijadala mbalimbali kila kona.
Sababu kubwa ya mijadala hiyo kutawala yaweza kuwa ni takriban kila familia
kuguswa kwa njia moja ama nyingine na matokeo hayo.
Katika matokeo hayo karibu shule zote za umma zimefanya vibaya, zile za kata
zikiongoza katika kufelisha, huku ile ya Mibuyuni iliyopo Kilwa mkoani
Lindi ikiwa ya mwisho kabisa katika kundi la shule zenye zaidi ya wanafunzi 40.
Mkuu msaidizi wa shule hiyo Robart Mzumbi, alisema kuwa matokeo
hayo yalitarajiwa kwa kuwa tangu wanafunzi hao walipoandikishwa kidato cha
kwanza, hawakuwa wamefaulu.
Alibainisha kuwa, matokeo ya kidato cha pili ya wanafunzi hao walipofanya mtihani wa taifa mwaka 2010, yalikuwa kiashiria kingine kwamba, hata kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wanafunzi hao hawatafanya vizuri.
Pamoja na hayo, Mzumbi anaeleza kwamba kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni
kuhakikisha wanafundisha watoto hao na mwisho wafanye vyema, matokeo hayo
yamewasikitisha kwa kiasi kikubwa.
Alitaja upungufu wa walimu na umaskini wa kipato kwa jamii
inayozunguka shule hiyo kuwa ni moja ya sababu kubwa zilizosababisha matokeo
hayo mabaya.
Mwalimu huyo alibainisha kwamba idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika
shule hiyo hujishughulisha zaidi na biashara ndogo ndogo, badala ya kusoma.
Aliweka wazi kuwa, shule hiyo ilikuwa ya mwisho kati ya shule 3,392 zenye watahiniwa 40 na kuendelea, wakati watahiniwa hao wa mwaka 2012 walipochaguliwa kuingia kidato cha kwanza mwaka 2009, ambapo walikuwa na alama za chini.
Aliongeza kuwa wanafunzi hao walichaguliwa kuanza kidato cha kwanza wakati
tayari wengi wao walishaanza kufanya biashara ndogondogo, hivyo walikusanywa
kutoka huko mitaani na kupelekwa shule.
“Ndugu yangu shule yetu huwa inafanya vizuri kidogo, angalia matokeo ya
kidato cha pili mwaka huu Sekondari ya Mibuyuni imekuwa ya 115 kati ya shule
242 za Kanda ya Kusini, wanafunzi wanane wamefaulu kati ya 25 waliofanya
mtihani. Lakini kwa matokeo ya kidato cha nne, kwa kweli wanafunzi
waliochaguliwa mwaka 2009, hawakuwa na sifa bali waliokotwa tu ili kujaza
darasa,” alisema na kuongeza:
“Hata mtihani wa kidato cha pili mwaka 2010, walifanya vibaya sana na
shule hii ilikuwa ya pili kutoka mwisho.”
Mzumbi alisema kwamba shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwamo kukosa maabara, upungufu wa walimu wa sayansi, usafiri na umeme wa
uhakika.
Pia ina ukosefu wa maji, nyumba za walimu, mabweni kwa ajili ya watoto wa kike, pamoja na shule kujengwa mbali na makazi ya wananchi.
Alieleza kuwa wanafunzi wengi wanaosoma katika shule mbalimbali za Mkoa wa
Lindi, hulazimika kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni.
Mohamedi Bori, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo anasema kuwa wakati shule
hiyo ilipofunguliwa mwaka 2008, ilikuwa na walimu wawili, kwa kipindi cha
zaidi ya miaka mitatu mfululizo.
Bori alisema kuwa wakati wao walipoingia kidato cha kwanza mwaka 2010,
kulikuwa na walimu watatu, huku shule hiyo ikiwa na wanafunzi 140
wa kidato cha kwanza hadi cha nne, hali ambayo ilisababisha walimu
kuelemewa na majukumu ya kufundisha.
Sababu nyingine za kufanya vibaya zinatajwa kuwa ni walimu wachache waliopo
kuondoka mara kwa mara na kukatisha mitalaa hivyo wanafunzi kutoshika vizuri
wanayofundishwa hali iliyochangia pia wanafunzi kukata tamaa na kuangukia
kwenye utoro.
Wanafunzi wengine walisema kuwa hali hiyo ilichangia wengi wao kuamua kujihusisha
na biashara ndogondogo ikiwamo ya kuuza samaki, migahawa, maji, biskuti
na juisi katika stendi kuu ya mabasi Nangurukuru.
Naye Saidi Mwichande, mkazi wa Kijiji cha Mkwajuni Nangurukuru, alisema kuwa wamepokea matokeo ya watoto wao kwa huzuni na kwamba wanatarajia kufanya kikao cha pamoja na walimu na wanafunzi wa shule ili kubaini tatizo lililopo.
Mwichande alisema jukumu la kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya shule hiyo lipo
mikononi mwa wazazi na wadau wengine wanaoishi katika kata hiyo ili kuiletea
maendeleo ya shule hiyo.
Wakati huohuo, Mawaziri wa zamani wa Serikali, Profesa Simon Mbilinyi aliyekuwa Waziri wa Fedha na Gaudence Kayombo aliyekuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji, wameelezea kusikitishwa kwao na idadi kubwa ya wanafunzi waliohitimu kidato cha nne 2012 kufeli mitihani yao.
Akizungumza katika mahojiano na gazeti hili, Mbilinyi alisema kuwa
matokeo hayo yamechangiwa na kushuka kwa nidhamu kwa walimu na wanafunzi huku
akiitaka Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wahitimu waliofeli.
“Mafanikio yoyote ya elimu yanachangiwa na nidhamu, naweza kusema tatizo la
matokeo mabaya limechangiwa na kushuka kwa nidhamu. Angalia, shule za misheni
mara nyingi zimekuwa zikifanya vyema kuliko shule za kata, au za Serikali. Hii
ni kutokana na wao kujali nidhamu hata mwanafunzi akiwa na akili za kutisha
akifanya utovu wa nidhamu hufukuzwa,”alisema Profesa Mbilinyi.
Alitoa ushauri kwa wazazi, walimu na jumuia zinazowazunguka wanafunzi
kuwajengea nidhamu ya kuheshimu masomo na kupenda kujisomea ili kuweza kutatua
tatizo la wanafunzi kufeli.
Kwa upande wake Gaudence Kayombo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki alisema taifa linahitaji kufanya utafiti ili kujua kilichochangia wanafunzi hao kufeli kwa kiwango kikubwa.
Alisema kuwa ili tatizo hilo lipatiwe ufumbuzi, wakaguzi wa elimu wana
wajibu wa kuwakagua walimu kama wanatimiza wajibu wao ipasavyo kwa
kuwafundisha wanafunzi, lakini pia Serikali itoe vifaa vya kufundishia
ili kuhakikisha wanafunzi wanapewa haki yao ya msingi ya kufundishwa na
kuelewa.
Aliwataka wazazi kutimiza wajibu wao kwa kuwabana na kukagua madaftari ya
watoto wao wanaporudi nyumbani ili kuwajengea moyo wa kupenda kujisomea.
chanzo mwananchi.
0 comments:
Post a Comment