Timu ya Taifa ya Tanzania
(Taifa Stars) imeendelea na mazoezi katika uwanja wa Olympia Park kujiandaa na
mchezo wa fungua dimba dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland.
Kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars Mart
Nooij amesema vijana wake wanaendelea vizuri na mazoezi, ikiwa leo ni siku ya
pili kufanya mazoezi baada ya kufanya mazoezi ya kwanza jana jioni.
Nooii amesema japokuwa kuna hali ya hewa ya
baridi katika mji wa Rustenburg, wachezaji wake wameanza kuizoea na kusema kwa
kuwa bado kuna zaidi ya masaa 72 kabla ya mchezo wa awali watakua wameshaizoea
hali ya hewa.
Kuhusu uwanja wa mazoezi, kocha Nooij
amesema hali ya uwanja ni nzuri, uwanja una nyasi nzuri hali inayopelekea
kikosi chake kufanya mazoezi katika mazingira mazuri.
Akiongelea mchezo wake wa kwanza wa
ufunguzi dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland utakaochezwa siku ya jumatatu,
amesema anawajua Swaziland ni timu nzuri, mara ya mwisho katika mchezo wa
kirafiki walitoka nao sare, hivyo anawaanda vijana wake kupata ushindi katika
mchezo huo.
Kikosi cha Swaziland kina wachezaji
mchanganyiko wakiwemo wanaocheza ligi yao ya nyumbani na baadhi wanaocheza soka
la kulipwa nchini Afrika Kusini.
Taifa Stars itacheza mchezo wa kwanza dhidi
ya Swaziland katika Uwanja wa Olympia Park siku ya jumatatu saa 1.30 usiku kwa
saa za huku, sawa na saa 2.30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
0 comments:
Post a Comment