02 Januari, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU PINDA APEWA TUZO YA MKOA WA KATAVI
*Ni tuzo mbili za mwaka katika utawala bora na ufugaji nyuki
*Atangazwa rasmi kuwa Mfalme wa Nyuki Tanzania
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepewa
Tuzo ya Heshima ya Mwaka 2012 ya Mkoa wa Katavi katika vipengele viwili vya
Utawala Bora na Uhamasishaji wa ufugaji nyuki.
Waziri Mkuu alipokea tuzo hizo
usiku wa kuamka jana (Jumanne, Januari Mosi, 2013) kwenye hafla ya kuuaga mwaka
2012 na kuukaribisha mwaka 2013 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Maji
mjini Mpanda, mkoani Katavi.
Akitoa maelezo ya utangulizi kabla
ya kutangaza majina ya watunukiwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi
Emmanuel Kalobelo alisema mkoa wa Katavi umeamua kuanzisha mfumo wa utoaji wa
Tuzo ya Mkoa kwa lengo la kuwatambua, kuwatia moyo na kuwapa motisha wananchi
na watumishi wa umma waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za utoaji wa
huduma kwa wananchi.
“Tuzo
hii itaendelea kutolewa kila mwisho wa mwaka... Tumeamua kufanya hivi ili
kuamsha ari kwa wengine kufanya vizuri zaidi mwaka unaofuata,” alisema.
Sekta
zilizopewa tuzo ni mapato na kodi za Serikali, utawala bora, uchumi na
maendeleo, Ulinzi na usalama, mipango miji, mawasiliano na teknolojia, ufugaji
nyuki na hifadhi ya mazingira, elimu, kilimo na mifugo, michezo, usafirishaji
na huduma za jamii.
“Waziri
Mkuu Mizengo Pinda anatunukiwa tuzo ya utawala bora, siasa safi na ushiriki katika
shughuli za maendeleo ya wananchi wa jimbo lake la Katavi na Ukanda wa Ziwa
Tanganyika kikamilifu,” alisema. “Tuzo
ya pili ni ya kumtambua kuwa mfugaji nyuki na mhamasishaji kichocheo wa kitaifa
wa ufugaji nyuki. Sisi wana-Katavi tunakutambua kama Mfalme wa Nyuki nchini,” aliongeza.
Wengine waliopewa tuzo katika hafla
hiyo ni Bw. Deus Assenga, Bw. Michael M. Tarimo
wa M.M (2001) Group Ltd na Bw. Shabir Hassanali Walimohamed ambao walitambuliwa
kama Walipakodi Bora Mkoa wa Katavi mwaka 2012 kwenye kipengele cha Mapato na
Kodi za Serikali.
Wengine
ni Bw. Paschal Kweya aliyepewa tuzo katika ubunifu wa usafi na hifadhi ya mazingira
Mkoa wa Katavi ambaye aliiwezesha Halmashauri ya Mji kuwa mshindi mara mbili
mfululizo 2011 na 2012.
Waliotunukiwa
tuzo kwenye kipengele cha mawasiliano na teknohama ni Bw. Majaliwa Rubuye
ambaye alibuni tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda yenye anwani ya www.mpandadc.go.tz na kuweza kuweka
daftari la mkulima katika mtandao huo. Bw. Ignas Kikwala ambaye ni Afisa
Maendeleo ya Jamii alibuni machapisho na kuandaa gazeti la Mpanda Leo ambalo hutolewa kila baada ya miezi mitatu. Hadi sasa
ametoa matoleo sita.
Walioshangiliwa
zaidi kwenye utaoaji tuzo hizo ni vijana watatu ambao walishiriki mashindano ya
Maisha
Plus wakitokea mkoa wa Katavi na wakafanikiwa kufika fainali za
mashindano hayo. Vijana hao ni Bi. Theresia Zacharia ambaye amepata nafasi ya
kujiunga na JKT moja kwa moja bila kufanyiwa usaili; Bw. Lucas Martin na Bw.
Gabriel Luvinga.
Waliotunukiwa
tuzo kwenye sekta ya elimu ni wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mtihani wa
darasa la saba ambao wanatoka kwenye shule za kawaida za Vijijini katika wilaya
ya Mpanda na wamechaguliwa shule za wenye vipaji maalum. Vijana hao ni Benjamin
Busagala (kutoka S/M Majimoto) ambaye amechaguliwa kwenda Sekondari ya Mzumbe
na Christina Boniface kutoka S/M Ikuba ambaye amechaguliwa kwenda sekondari ya
wasichana Tabora
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JANUARI 02, 2013.
Irene K. Bwire,
Email: irenekaki@yahoo.com
"The secret to success is constancy to purpose"
0 comments:
Post a Comment