Main Menu

Sunday, December 15, 2013

WAHITIMU CHUO KIKUU MZUMBE MBEYA WASHAURIWA KUWA WAPAMBANAJI


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Joseph Kuzilwa (kulia) akiwa pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Prof. Daniel Mkude (katikati) na Prof. Gerald Monela wakati wa mahafali ya 12 ya chuo hicho, kampasi ya Mbeya mwishoni mwa wiki jijini Mbeya.
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, kampasi ya Mbeya, Prof. Ernest Kihange akiwa pamoja mkuu wa chuo hicho kampasi ya Dar es Salaam, Prof. Andrew Mbwambo (kushoto kwake) wakati wa mahafali ya 12 ya chuo hicho, kampasi ya Mbeya mwishoni mwa wiki jijini Mbeya.

Vijana wahitimu wa vyuo vikuu wameshauriwa kuingia katika soko la ajira wakiwa wanajiamini na kujipambanua kiuwezo kutokana na elimu waliyopata wakiwa chuoni.

Akiongea wakati wa mahafali ya 12 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Mbeya jijini humo mwishoni mwa wiki, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Joseph Kuzilwa alisema kuwa vijana wahitimu hasa toka chuo hicho wanatakiwa kuonyesha kuwa wanaweza kazi kwa kuwa elimu waliyopata ni bora na iliwatayarisha kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Alifafanuwa kuwa pamoja na changamoto za ajira zilizopo nchini, bado nafasi zipo ila kinachotakiwa kwa vijana ni kujiamini na kutumia vizuri elimu waliyopata kwa faida yao nay a nchi.
“Vijana waingie katika soko wakiwa wapambanaji na sio watu walioshindwa,” alisema.

Akitoa ushauri zaidi alisema vijana hao watumie pia fursa za kujiajiri na biashara kwa kutumia vizuri elimu na maarifa ya ujasiriamali waliyopata chuoni.

Alisema katika azma ya kutoa elimu bora zaidi na kutoa wahitimu wenye uwezo mzuri kiutendaji na kifikra, chuo hicho kimeanzisha mikakati ya kuboresha njia za kielektroniki na kampasi ya Mbeya ikihusishwa.

Alisema tayari wahadhiri wa kampasi hiyo wamepewa mafunzo kuhusu njia hizo na bado mafunzo yanaendelea kwa wanafunzi pia.
“Njia hizi mpya zinafaa hasa kwa kipindi hiki ambacho vyuo vingi sasa vinapanuka kwa idadi ya wanafunzi,” alisema.

Pamoja na kuishukuru serikali kwa mafanikio ya kampasi hiyo, pia aliiomba pamoja na wadau wengine wa elimu ya juu, kuongeza juhudi katika kushirikiana na chuo kukabiliana na changamoto zinazokabili chuo.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Gerald Monela, alisema uongozi utaendelea kuipanua kampasi hiyo ili kuongeza nafasi zaidi kwa wadau wengi wanaopenda kupata elimu katika chuo hicho.

Alisema mpango wa kukamilisha taratibu za umiliki wa eneo la Iwambi kwa ajili ya upanuzi wa kampasi hiyo unaendelea vizuri na kuwa mara baada ya kukamilisha taratibu za umiliki, mikakati ya upanuzi itaanza.

“Tunahitaji sana ushirikiano mkubwa na wananchi wa mkoa wa Mbeya na wadau wengine katika kutimiza azma hii,” alisema, huku akiushukuru uongozi mzima wa jiji la Mbeya na wananchi wake kwa kuwapatia eneo hilo.

Aliwaasa wahitimu wote kujihadhari na janga la ukimwi na madawa ya kulevya ili taifa lisipoteze nguvu kazi adimu iliyowekezwa ndani yao.

Jumla ya wahitimu 567 walitunukiwa shahada mwaka huu kulinganisha na 314 mwaka jana katika programu za astashahada, 235; stashahada, 121; shahada ya kwanza, 173 na shahada ya uzamili, 38.

Kampasi ya Mbeya imeendelea kukua kwa idadi ya wanachuo ambayo imeongezeka kutoka 405 mwaka 2006 hadi kufikia 2241 mwaka huu, hii ikiwa ni ongezeko la takribani asilimia 453.


0 comments:

Post a Comment