Main Menu

Tuesday, August 6, 2013

HUU NDIO USAJILI WA VILABU VYOTE VYA LIGI TANZANIA BARA

 KWA mujibu wa kalenda ya matukio ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hatua ya kwanza ya uhamisho wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu Bara imefungwa rasmi usiku wa kuamkia leo Jumanne ingawa itafunguliwa tena kwa muda wa wiki mbili kuanzia Agosti 15, mwaka huu.

Kila klabu ilikuwa kwenye pilikapilika za kuhakikisha inafanya usajili mzuri na kujenga kikosi chake kuwa imara kwa ajili ya msimu ujao wa ligi. Kama si kutwaa taji la ubingwa wa ligi hiyo, basi kumaliza katika nafasi tatu za juu ama kutoshuka daraja ili iwepo kwa msimu mwingine.

Azam FC ndiyo timu pekee ambayo haijafanya usajili wa mchezaji yeyote mpya badala yake imepandisha vijana watatu kutoka kwenye timu yake ya vijana U-20.

Yosso hao ni makipa Aishi Manula na Hamad Juma na kiungo aliye kwenye kikosi cha Taifa Stars pamoja na Manula, Mudathir Yahya.
Ifuatayo ni orodha ya majina ya wachezaji wapya katika klabu zote 14 za Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao utakaoanza kutimka Agosti 24, mwaka huu.

Yanga SC
Imesajili wachezaji saba wapya ambao ni Hamis Thabit (huru), Deogratius Munishi ‘Dida’ (huru), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Reliant Lusajo (Machava United, Kilimanjaro), Shaaban Kondo (huru), Rajabu Zahir (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngassa (Azam/Simba). Lakini kama ilivyo Simba inamfukuzia raia wa Uganda, Mosses Oloya.

Simba SC
Simba na Ashanti United ndizo timu pekee ambazo zimeongoza kusajili wachezaji wengi wapya. Simba imesajili kikosi kizima cha wachezaji 10 wapya huku kama Yanga ikimfukizia raia wa Uganda, Moses Oloya.
 Wapya hao ni Abdulhalim Humoud (huru), Issa Rashid (Mtibwa Sugar) Ibrahim Hussein (Coastal Union), Adeyoum Saleh (Miembeni, Zanzibar), Sino Agustino (Prisons Mbeya), Andrew Ntalla (Kagera Sugar), Joseph Uwino (URA, Uganda), Rahim Juma (huru), Amis Tambwe (Vital’O, Burundi) na Kaze Gilbert (Vital’O,Burundi).

Azam FC
Haijafanya usajili wowote mpya ingawa imepandisha vijana watatu kutoka kikosi cha timu yake ya vijana. Yosso hao ni Mudathir Yahya, Aishi Manula na Hamad Juma.


Coastal Union
Imeongeza wachezaji wapya nane ambao ni Juma Nyosso, Haruna Moshi wa Simba  na Uhuru Seleiman kutoka Azam. Wengine ni Kenneth Masumbuko (Polisi, Moro), Crispian Odulla (Bandari, Kenya), Abdullah Othman (Jamhuri ya Pemba), Marcel Ndaheli na Said Rubawa kutoka Oljoro JKT ya Arusha.

Mtibwa Sugar
Walioiona kwenye Uwanja wa Taifa ilipopoteza kwa mabao 3-1 kwenye mechi ya kirafiki na Yanga Jumapili iliyopita wamekiri kwamba inacheza soka safi na huenda ikatisha zaidi msimu ujao tofauti na baadhi wanavyodhani.

Mtibwa ambayo imekuwa ikiporwa wachezaji kila wakati na vigogo wa soka Simba na Yanga imesajili wachezaji watano wapya. Nyota hao ni Paul Ngalema, Abdallah Juma kutoka Simba na kipa  Said Mohamed aliyetemwa na Yanga.

Wengine ni beki Salim Mbonde kutoka Oljoro JKT na winga Ally Shomari aliyekuwa akikipiga na Polisi Moro iliyoshuka daraja.

Kagera Sugar
Imesajili wachezaji watano wa bei chee. Nyota hao ni wale klabu zao zilishuka daraja msimu ulioisha ambao ni Musa Said, Erick Mlilo,Peter Mutabuzi na Seleiman Kibuta kutoka Toto Afrika ya Mwanza na kipa Aghaton Antone wa Polisi, Morogoro

Ruvu Shooting
Ni moja kati ya timu ambayo imesajili vizuri na inatabiriwa kutisha msimu ujao wa ligi. Imesajili wachezaji saba wapya ambao ni Elius Maguri (Prisons Mbeya), Juma Nade (Kagera Sugar), Jerome Lambele (Ashanti United), Cosmas Lewis na Seif Abdul (African Lyon), Juma Seif ‘Kijiko’ na Stephano Mwasika kutoka Yanga.


JKT Ruvu
Kocha mpya Mbwana Makatta amekuja na staili yake mpya kuwekeza kwenye soka la vijana. JKT iliyonusurika kushuka daraja imesajili wachezaji watatu wazoefu ambao ni
Emmanuel Swita (Toto African)
Kalage Gunda (Oljoro JKT) na Salum Machaku (Polisi Moro)

Tanzania Prisons
Kocha msaidizi Oswald Morris ametamka kuwa wamefumua kikosi chao na kukisuka upya kwa kuongeza damu changa. Ingawa wamechanganya kidogo na wazoefu kipa Wilbert Mweta (Simba)Ibrahim Mamba (Oljoro JKT) na
Omega Seme (Yanga, mkopo)

Mbeya City
Itakuwa inashiriki kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Soka Tanzania Bara tangu kuanzishwa kwake. Kocha Juma Mwambusi amesajili wachezaji watano wapya ambao ni Paul Nonga (Oljoro JKT), David Abdallah (Prisons Mbeya), Mohamed Kijuso (huru), Christian Sembuli (Polisi,Dodoma) na John Paul (Polisi, Moro)

Oljoro JKT
Imemrejesha kundini straika wake Amir Omary aliyetimka mzunguko wa pili kwa madai ya kutolipwa fedha za usajili wake na kiungo aliyemaliza mkataba wake na Mtibwa Sugar Babually Seif. Pia, imepandisha vijana 18 kwenye kikosi chake.

Ashanti United

Imejiopanga upya kuanzia kwenye beBenchi lake la ufundi limekataa kuchukua wachezaji kutoka klabu kongwe za Simba na Yanga. Imesajili kikosi kizima kipya. Nyota hao ni Anthony Matangalu (huru),
Issa Kanduru na Salum Malima kutoka (Mgambo JKT), Tumba Sued (huru) Hussein Sued (Ruvu Shooting), Said Maulid ‘SMG’ (huru), Daudi Mwasongwe (Prisons, Mbeya) Raul Magia (Polisi Moro), Musa Chibwabwa (Villa Squad) na Paulo Maono (Moro United)

Rhino Rangers
Uongozi wa timu hiyo umemtimua Kocha Renatus Shija aliyeipandisha Ligi Kuu timu hiyo na kumpa mikoba hiyo aliyekuwa kocha wa Jamhuri ya Pemba, Sebastian Nkoma.
Imewasajili wachezaji wawili kutoka Yanga, Nurdin Bakari na Ladislaus Mbogo ambao wataiongezea uzoefu ingawa haikufanya vizuri sana kwenye mechi za kirafiki kujiandaa na msimu mpya.

Mgambo JKT
Kocha Mohamed Kampira amesema klabu hiyo haikuwa na fedha za usajili wachezaji wenye majina makubwa na kuweka nguvu zao kwenye vijana.

“Tumesajili wachezaji wengi vijana ambao hawana majina katika soka.Tunataka kutoka nao kutoka huku chini kupanda nao,” alisema Kampira ambaye amesisitiza kuwa msimu huu watatoa ushindani mkubwa na wamesajili timu ya kucheza soka la uhakika na kutafuta matokeo si kama ilivyokuwa misimu iliyopita.

NA MWANASPOTI

0 comments:

Post a Comment