Main Menu

Wednesday, May 1, 2013

TAARIFA KUTOKA TFF, MIKOA 18 YAPATA MABINGWA WA MIKOA


Mikoa 18 kati ya 27 ya kimpira tayari imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Timu tatu za juu katika Ligi hiyo ya Mabingwa zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014). Ligi ya FDL ina jumla ya timu 24 ambapo tatu katika ligi hiyo zilizoshuka daraja msimu huu ni Moro United ya Dar es Salaam, Small Kids ya Rukwa na Morani FC ya Manyara.

Mabingwa waliopatikana hadi sasa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).

Wengine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).

Kila klabu inatakiwa kulipa ada ya ushiriki ambayo ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.

MTANZANIA AOMBEWA ITC ACHEZE NORWAY
Shirikisho la Mpira wa Miguu Norway (NFF) limetuma maombi ya kupatiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Godfrey Mlowoka ili aweze kucheza mpira nchini humo.

NFF inamuombea hati hiyo Mlowoka ili aweze kujiunga na klabu ya Ekne IL kama mchezaji wa ridhaa ambapo klabu yake ya zamani aliyokuwa akiichezea nchini imetajwa kuwa Sadani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanyia kazi maombi hayo na mara taratibu zote zitakapokamilika hati hiyo ya uhamisho itatumwa nchini Norway.

AZAM YAENDELEA KUJINOA MOROCCO
Timu ya Azam ambayo iko jijini Rabat kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabati ya huko inaendelea vizuri na mazoezi.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari Msaidizi wa Azam FC, Jaffer Idd maandalizi yanakwenda vizuri kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi (Mei 4 mwaka huu). Jaffer Idd anapatikana kwa namba +212671146092.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment