Main Menu

Tuesday, April 23, 2013

SPIKA ASIPOTENDA HAKI BUNGE HALITAKALIKA

Leo tumelazimika tena kuzungumzia hatima ya Bunge la 10, baada ya hadhi yake kuendelea kudidimia kwa kasi ya ajabu. 

Tumeendelea kushuhudia baadhi ya wabunge wakitoa lugha za kihuni na kibazazi na kuligeuza Bunge kuwa jukwaa la wabunge waliochanganyikiwa.

Tumekuwa tukionya mara kwa mara kwamba hali hiyo inahatarisha demokrasia ndani ya Bunge ambalo katika macho ya wengi limekuwa likiendeshwa kinyume na matarajio ya kuanzishwa kwake. 


Mara zote tulipokemea hali hiyo tulikataa kutafuna maneno, hivyo tulisema waziwazi na kwa nia njema tu kwamba Kiti cha Spika kinayumba kwa namna ambayo haina mfano wake tangu nchi yetu ipate Uhuru.

Historia ya maspika wa Bunge letu tangu tupate uhuru ni ya kujivunia. Maspika waliopita, ingawa wengi wao waliliongoza Bunge wakati nchi yetu ikiwa chini ya mfumo wa chama kimoja walijitahidi kukiongoza chombo hicho kwa kufuata Kanuni za Bunge, hivyo kulifanya Bunge liwe na heshima na hadhi stahiki mbele ya wananchi na wabunge wake.

Lakini hata baada ya ujio wa siasa za vyama vingi mwaka 1993, Bunge liliendelea kupata hadhi hiyo. 


Maspika Pius Msekwa na Samwel Sitta walifanya kazi nzuri ya kuendelea kulinda hadhi ya Bunge na kuwaunganisha wabunge.
Pamoja na maspika hawa kuwa wanachama wa CCM, maamuzi yao kuhusu masuala yote ya msingi kwa masilahi ya taifa letu yalifanywa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge pasipo kuonea wabunge wa Upinzani wala kupendelea wabunge wa chama chao. 


Ndiyo maana amani ilitamalaki bungeni na chombo hicho kikaendelea kuheshimiwa ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, hapa lazima tusisitize jambo moja. Kwamba mfumo wa kikatiba ambao unawataka maspika wa Bunge watokane na vyama vya siasa pia uliwakwaza maspika Msekwa na Sitta kwa namna fulani. Lakini yalipokuja masuala ya kitaifa yahusuyo mustakabali wa nchi yetu, maspika hao waliweka mbele masilahi ya taifa badala ya itikadi za vyama.

Haikutokea hata siku moja wakapindisha au kuvunja Kanuni za Bunge makusudi kwa lengo la kukipendelea CCM au wabunge wake kama tunavyoshuhudia hivi sasa Spika Makinda na wasaidizi wake wakifanya mchana kweupe.

Tulishuhudia bungeni siku chache zilizopita baadhi ya wabunge wa CCM wakiporomosha matusi yasiyotamkika na kukingiwa kifua na Kiti cha Spika, lakini wakati huohuo kiti hicho kikiwasimamisha kwa siku tano kuhudhuria vikao vya Bunge baadhi ya wabunge wa Upinzani walioomba mwongozo wa Spika wakilalamikia matusi hayo.

Kwa hali hiyo, tusitegemee amani itamalaki bungeni kama Kiti cha Spika kitaendelea kupwaya na kushindwa kutoa haki kwa kuendekeza maamuzi ya undumila kuwili. 



Pengine kosa kubwa lililofanywa na CCM ni kumwengua Spika Sitta kwa kudhani Spika Makinda angekisaidia zaidi chama hicho bungeni pasipo kujua kuwa, tofauti na mtangulizi wake, Spika Makinda hakuwa na karama wala uwezo wa kuliongoza Bunge.

Maoni ya wananchi wengi, wakiwamo wasomi, wanasiasa, wanafunzi, vyama visivyo vya kiserikali, wanaharakati na vyama vya wafanyakazi ni kwamba Spika Makinda amedhoofisha na kudidimiza hadhi ya Bunge kuliko spika yeyote katika historia ya nchi yetu. Bunge hili linahitaji uongozi na mwelekeo mpya.


Vinginevyo, Spika Makinda ataendelea kutuhumiwa anaendeshwa kwa ‘rimoti’ kutoka nje ya Bunge.

chanzo mwananchi.

0 comments:

Post a Comment