Okwi alitua kwa ndege ya RwandaAir Saa 9:55 jioni na kulakiwa na viongozi na wapenzi kadhaa wa timu hiyo JNIA kabla ya kupakiwa kwenye gari ndogo aina ya saluni alilokuwa akiendesha Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga, Seif Ahmed ‘Magari’ na kuondoka.

Okwi alitokea geti la wageni maalum la JNIA na kusindikizwa na Polisi huku, umati wa mashabiki wa Yanga ukimshangilia na kumfanya atoke kwa taabu hadi kupanda gari.
Mara tu baada ya kutoka nje ya JNIA, Okwi alisema; “Nimekuja Yanga kufanya kazi,” na alipoulizwa kuhusu utata wa usajili wake, akasema; “Mimi nimekuja kufanya kazi, hayo mengine, mamlaka husika zitajua,”alisema Okwi aliyekuwa amevalia jezi nambari 25 ya Yanga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdaollah Ahmed Bin Kleb alisema kwamba mchezaji huyo anakwenda moja kwa moja kambini, Protea Hotel kuungana na wenzake tayari kwa mchezo wa Jumamosi wa Nani Mtani Jembe dhidi ya mahasimu, Simba SC.

Simba na Yanga zitamenyana Jumamosi katika mchezo ambao iwapo dakika 90 zitamalizika kwa sare, mikwaju ya penalti itaamua mshindi.
Mchezo huo, unaoandaliwa na wadhamini wa klabu hizo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, unatarajiwa kuchezeshwa na refa Ramadhan Ibada ‘Kibo’ kutoka Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na Simon Charles kutoka Dodoma, wakati refa wa akiba atakuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam na mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi wa Arusha.
0 comments:
Post a Comment