Manyele ameipinga kauli iliyotolewa na Taasisi ya
Saratani ya Ocean Road mwanzoni mwa wiki hii kwamba mafuta hayo hayana
madhara katika mwili wa binadamu yakitumiwa vizuri.
Juzi, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Seif Rashid, alitangaza kuwa mafuta hayo si salama na kusisitiza kuwa
huo ndiyo msimamo wa Serikali kuhusu mafuta hayo, hivyo wananchi waamue
wenyewe kuyatumia au kutokuyatumia.
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Manyele
alisema, “ Ofisi yangu inaiunga mkono kauli ya Mamlaka ya Chakula na
Dawa nchini (TFDA) kuzuia matumizi ya mafuta hayo, Watanzania wanatakiwa
kuwa wasikivu na onyo hilo.”
Alisema sheria inayoruhusu mtu yoyote kufanya biashara ya chakula na dawa ipo chini ya TFDA, wao ndio wanaotoa
kibali cha kufanya biashara na kutengeneza bidhaa, kwamba wakisema
bidhaa fulani haifai wanatakiwa kusikilizwa.
“Wao ndio wanaotoa kibali cha kutengeneza bidhaa,
pia wana uwezo wa kuzuia uzalishaji kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya
Mkemia Mkuu haiwezi kuzuia uzalishaji,” alisema
Alisema tayari TFDA imeshaeleza athari ya kemikali
iliyopo katika mafuta ya ubuyu inayoweza kuathiri afya ya Watanzania,
kuwataka wananchi kuwa makini na kama wanahitaji taarifa za msingi
wanatakiwa kwenda katika ofisi za Mamlaka hiyo.
“Mimi kama Mkemia Mkuu wa Serikali nitaingilia
kati kama mambo yote yatashindikana na Serikali itataka kutoa tamko
rasmi kuhusu matumizi ya mafuta haya,” alisema
Hivi karibuni, TFDA ilipiga marufuku matumizi ya
mafuta ya ubuyu kwa madai kuwa yanasababisha saratani, tamko ambalo
lilipingwa vikali na wataalamu wa tiba mbadala.
Daktari Bingwa wa Udhibiti wa Saratani, katika
taasisi ya Ocean Road, Dk Crispin Kahesa juzi alizungumza na gazeti moja
la kila siku (sio Mwananchi) mafuta hayo ni salama kwa matumizi ya
binadamu, kama yakitumiwa vizuri.
Alisema mafuta ya ubuyu siyo dawa bali yanazuia
maradhi sugu yasiyoambukiza, yakiwamo saratani kwa sababu kitaalamu yana
‘ant oxidant’ (uchachu) ambao pia hupatikana kwenye baadhi ya matunda
kama maembe, machungwa na mananasi.
Kitendo cha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kutangaza kuwa
mafuta hayo ni salama iwapo yakitumiwa vizuri, pamoja na mwendelezo wa
malalamiko kutoka kwa wananchi na wataalamu mbalimbali, limekuwa likizua
utata kwa kuwa kila upande unaonekana kutoa msimamo wake jambo ambalo
limeibua mjadala katika jamii.
Tamko TFDA
TFDA ilitoa taarifa kuhusu matumizi ya mafuta ya
ubuyu na kueleza kuwa yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina
ya cyclopropenoic fatty acids ambayo huweza kusababisha athari ya kiafya
endapo mafuta hayo yatatumika kama chakula.
Ilieleza kuwa kiwango cha tindikali hiyo huweza tu
kupunguzwa katika mafuta ya mbegu za ubuyu kwa kuchemsha mafuta hayo
katika nyuzi joto 180 kwa muda wa saa nane au kwa kutumia teknolojia ya
kutengeneza mafuta mgando (hydrogenation).
“Kwa sasa hapa nchini hakuna aina ya usindikaji
unaofanyika wenye uwezo wa kuondoa tindikali ya cyclopropenoic fatty
acids katika mafuta ya mbegu za ubuyu” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ilieleza kwamba baadhi ya athari zinazoweza
kutokana na matumizi ya mafuta ya ubuyu ni pamoja na kuathiri
vimeng’enyo (enzymes) vinavyosaidia katika uchakataji wa tindikali za
mafuta mwilini (fatty acid biosynthesis).
NA gazeti mwananchi.
NA gazeti mwananchi.
0 comments:
Post a Comment