Main Menu

Wednesday, August 14, 2013

JAJI MSTAAFU KUTOA USHAHIDI JARIBIO LA KUTAKA KUMTAPELE DR SLAA


Katibu Mkuu wa Chadema,Dk Willbrod Slaa.  


Jaji Mkuu Mstaafu,Barnabas Samatta ni miongoni mwa mashahidi 12 watakaotoa ushahidi katika kesi ya jinai ya jaribio la kumtapeli Katibu Mkuu wa Chadema,Dk Willbrod Slaa.

 
Wengine watakaotoa ushahidi katika kesi hiyo inayomkabili Abedi Adam Abedi (22) ni Dk Slaa mwenyewe na Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema.

Orodha ya majina ya mashahidi hao ilitolewa mahakamani juzi mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Denis Mpelembwa na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Maghela Ndimbo.

Wengine watakaotoa ushahidi ni wakili mashuhuri wa Chadema, Profesa Abdalah Safari, Rumisha Slaa, Happynes Masue, Godfrid Njau, Gervas Geneya, Neema Godbless,Aron Misanga, Prosper Mbilinyi na Judith Mashashi.

Akisoma maelezo ya awali, Ndimbo alidai kuwa kati ya Aprili na Mei, 2012, mshtakiwa alijitambulisha kwa Dk Slaa, Lema na Profesa Safari kuwa yeye ni mtumishi wa Takukuru.

Ilidaiwa kuwa katika kipindi hicho, mshtakiwa aliwapigia simu Dk Slaa, Lema na Profesa Safari na kujitambulisha kuwa yeye ni Abel Kibaso Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Ulanga.

Katika kipindi hicho pia, mshtakiwa aliwapigia simu viongozi hao akijitambulisha ni Jaji mstaafu Samatta akitaka wampe pesa ili washinde katika kesi iliyokuwa mahakama ya Rufaa.

Rufaa hiyo namba 47/2012 ilifunguliwa na Lema dhidi ya Mussa Hamisi na wenzake akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Arusha ya kupinga kuvuliwa Ubunge wa Arusha mjini kesi ambayo kwa sasa ilishatolewa uamuzi.

mashtaka huyo alidai mahakamani kuwa mshtakiwa alijifanya ni Jaji Mkuu Mstaafu Samatta wakati akijua siyo Jaji Samatta kwa lengo tu la kujipatia fedha kinyume cha sheria.

Hata hivyo Lema alishinda Rufaa hiyo na kurudishiwa Ubunge wake.

Mshtakiwa amekanusha mashtaka hayo na kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa rasmi Septemba 25 ambapo Jaji Samatta ni miongoni mwa mashahidi wa upande wa Jamhuri.

NA gazeti mwananchi

0 comments:

Post a Comment