Main Menu

Tuesday, June 4, 2013

RASIMU YA KATIBA YAKAMILIKA, VITI MAALUM VYAPIGWA CHINI, BUNGE LAPUNGUZWA, UMRI WA RAIS MIAKA 40.

Rasimu ya Katiba Mpya iliyozinduliwa jana, imependekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais wa Tanzania maeneo tofauti ya utendaji wake, ukiwamo uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali. 


Tume hiyo inapendekeza kwamba Rais ashirikiane na mihimili mingine ya dola katika uteuzi huo, huku ikiwataja Mawaziri na Naibu Mawaziri, Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi kuwa uteuzi wao utakapofanywa na Rais lazima uthibitishwe na Bunge.

Mapendekezo hayo ni tofauti na hali ilivyo sasa wakati uteuzi unaofanywa na Rais hauthibitishwi na Bunge, isipokuwa nafasi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais itapotokea ikawa wazi kwa sababu zozote zile.

Pia, tume inapendekeza Rais ashauriane na chombo kipya kitakachoundwa cha Baraza la Ulinzi la Taifa kuwateua viongozi wote wa taasisi za ulinzi nchini.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema mfumo wa utawala utaendelea kuwa kama ulivyo hivi sasa na kwamba, Rais ndiye mtendaji wa Jamhuri ya Muungano na atachaguliwa moja kwa moja na wananchi.

Jaji Warioba alisema Tume imependekeza mgombea urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kwamba, kinga ya kutokuhoji matokeo ya uchaguzi mahakamani iondolewe.

“Mgombea urais anaweza kupendekezwa na chama cha siasa au kuwa mgombea huru, mgombea wa nafasi hiyo atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa,” alisema Jaji Warioba na kuongeza: “Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kulalamikiwa mahakamani, lakini siyo kila mtu anaweza kufungua kesi, wanaoweza kufungua kesi ni wagombea urais na Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na mamlaka na uwezo wa kusikiliza malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima liamuliwe ndani ya mwezi mmoja, yaani siku 30.”

Alisema Tume inapendekeza Rais achaguliwe moja kwa moja na wananchi na kwamba, suala la umri pia lilijadiliwa kwa upana.
“Wengine walisema umri wa mtu kuruhusiwa kugombea urais uwe miaka 35 au 50 na kuendelea, Tume imeyachambua maoni yote na ikafanya utafiti kwa kupitia Katiba za nchi zingine ,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:

“Wengi walioomba kugombea nafasi hiyo walikuwa na umri wa miaka 40 au zaidi, kwa kuzingatia maoni ya wananchi, utafiti na hali halisi, Tume imependekeza Rais aendelee kuchaguliwa na wananchi pamoja na sifa nyingine mtu atakayegombea Urais asiwe chini ya miaka 40.”

Kutokupunguzwa kwa umri wa urais kutakuwa ni pigo kwa wansiasa vijana nchini waliopendekeza ushushwe na kuwa miaka 35, akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Zitto, Makamba watoa kauli.


Akizungumzia suala hilo jana, Zitto alisema uamuzi huo wa umri hana la kusema, kwa sababu yaliyotolewa ni mapendekezo ya Tume na kwamba, Chadema watatoa kauli baada ya viongozi kuwasiliana.
Kwa upande wake, Makamba iwapo amebadili msimamo wake, alisema: “Suala la umri siyo kigezo pekee cha kupata uongozi mzuri.”

Makamba alisema ujana wala uzee siyo kigezo cha kumnyima mtu uongozi.

Siku za nyuma Makamba, ambaye ni Mbunge wa Bumbuli, aliwahi kunukuliwa akitaka umri wa kugombea urais uwe miaka 35 badala ya 40 ya sasa.

Alisema suala la umri lisingemwathiri binafsi, kwani mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 41.

“Ninapongeza Watanzania kwa kutoa maoni yao na kutaka vijana kupewa nafasi za uongozi,” aliongeza Makamba. 

VITI MAALUM VYAPIGWA CHINI   
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imependekeza katika rasimu ya Katiba Mpya ukomo wa wabunge na kufutwa kwa nafasi za Viti Maalumu bungeni.

 
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu Joseph Warioba alisema jana, wanapendekeza kwamba ubunge uwe na ukomo wa vipindi vitatu vya miaka mitano, mitano akimaanisha kwamba kipindi cha mtu kuwa mbunge hakiwezi kuvuka miaka 15.

Rasimu hiyo ya Katiba imependekeza kutokuwapo tena kwa Viti Maalumu na badala yake, imetaka kuwapo kwa nafasi tano za uteuzi zibaki kwa Rais ambazo zitahusisha makundi maalumu ya watu wenye ulemavu pekee.

Jaji Warioba alisema Tume imependekeza kuwapo kwa majimbo 25 ya uchaguzi kwa Tanzania Bara na 20 kwa Zanzibar ambayo kila moja litakuwa na wabunge wawili, mwanamke na mwanamume. 


Kwa mujibu wa rasimu hiyo, majimbo hayo ni mikoa 25 ya Tanzania Bara na wilaya 10 za Zanzibar. Kwa maana hiyo, Bunge la Muungano litakuwa dogo lenye wabunge 75.

Mwenyekiti huyo alisema, wananchi watakuwa na mamlaka ya kumwondoa madarakani mbunge wao endapo hawataridhishwa na utendaji kazi wake.

Alisema hakutakuwa na uchaguzi mdogo wa wabunge kwa wabunge watakaopitia kwenye vyama vya siasa na badala yake jimbo litakapokuwa wazi chama kilichokuwa kikiongoza kitateua atakayeshika wadhifa huo.

“Uchaguzi mdogo utafanyika pindi tu aliyekuwa akiongoza alitokana na mgombea huru (binafsi) hivyo, Tume huru ya Uchaguzi itatakiwa kuandaa uchaguzi mdogo,” alisema Jaji Warioba.

Kuhusu kiti cha Spika na Naibu Spika, alisema baada ya kupokea maoni na wananchi mbalimbali, Tume hiyo imependekeza viongozi hao wasitokane na vyama vya siasa.

Alisema Tume inapendekeza Spika na Naibu Spika wasitokane na wabunge na wasiwe viongozi wa vyama vya siasa wala wasitokane na asasi za kiraia ambao wataidhinishwa na Bunge.

WANANCHI WAFURAHIA MAPENDEKEZO
Mkazi wa Uhindini, Mbeya, Boniface Mwakinga alisema amefurahishwa na mapendekezo yanayotaka kuwapo kwa ukomo wa madaraka ya wabunge.

Mfanyakazi wa Hospitali ya Kilema, Kilimanjaro, Dennis Mfumbulwa alisema kati ya mambo yaliyomgusa katika rasimu hiyo ni hatua ya wananchi kupewa nguvu ya kumwondoa mbunge ambaye hawajibiki kwa wapigakura wake akisema hilo sasa ni kitanzi kwa wabunge wababaishaji.

Mbunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki, Shyrose Bhanji alieleza kufurahishwa kwake na kuondolewa kwa Viti Maalumu na kupendekezwa kwa utaratibu mpya wa kusimama na kugombea wanawake majimboni.


 “Lengo la kuanzishwa Viti Maalum ilikuwa ni kuwapa upendeleo maalumu wanawake kuingia katika siasa na vyombo vya uamuzi, nadhani imefanikiwa na sasa tunapaswa kushindanishwa sisi kwa sisi,” alisema Bhanji.

mwananchi.

0 comments:

Post a Comment