Maelfu ya wakazi wa mkoa wa Mtwara na vitongoji vyake leo wamefanya
maandamano ya amani wakipinga mpango wa serikali ya Tanzania wa
kusafirisha gesi asilia iliyoko mkoani humo kwa kutumia mabomba hadi Dar
es Salaam.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango yenye kuelezea
jumbe na hisia zao, wameanza maandamano hayo asubuhi katika maeneo ya
Mtawanya na kuelekea Mtwara mjini.
Madai ya wananchi wa Mtwara ni pamoja
na kutaka gesi hiyo asilia isipelekwe moja kwa moja hadi Dar es Salaam,
kijengwe kiwanda cha gesi na wenyeji wapewe kipaumbele katika ajira na
makampuni ya kuchimba gesi yatoe huduma za kijami kama vile maji, afya,
elimu na barabara katika maeneo husika.
Taarifa zinasema kuwa, kinyume
na maandamano yaliyowahi kufanyika katika mikoa mbalimbali hivi karibuni
nchini humo, maandamano ya wananchi wa Mtwara hayakugubikwa na ghasia
wala machafuko, ingawa askari polisi walitanda pambizoni mwa
waandamanaji ili kuhakikisha unakuwepo usalama wa wananchi na mali
zao.
Wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kwa miaka kadhaa wamekuwa
wakilalamika kwamba, mikoa hiyo iko nyuma kimaendeleo kulinganisha na
mikoa mingine.
Rais Jakaya Kikwete alizindua rasmi ujenzi wa bomba hilo Novemba 8, mwaka huu
katika eneo la Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
chanzo, idhaa ya kiswahili radio tehrani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment