Main Menu

Wednesday, April 17, 2013

AS FAR RABAT YA MOROCCO SASA KUTUA SAA 7


TIMU ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayoikabili Azam kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho inatua nchini leo (Aprili 17 mwaka huu) saa 7.30 mchana kwa ndege ya Qatar Airways.

Msafara wa timu hiyo wenye watu 28 kwa ajili ya mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utafikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo.

Wakati Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1, AS FAR Rabat imeingia raundi hiyo moja kwa moja kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri kwenye michuano ya klabu Afrika.

Timu nyingine ambazo zimeingia raundi hiyo moja kwa moja katika Kombe la Shirikisho kama ilivyo AS FAR Rabat ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Atletico Petroleos (Angola), C.S.S. (Tunisia), DC Motema Pembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Ahly Shandy (Sudan), Enppi (Misri), Heartland (Nigeria), Ismaily (Misri), Lobi Stars (Nigeria), U.S.M. Alger ya Algeria na Wydad Casablanca (Morocco).

Mwamuzi Emile Fred atakayesaidiwa na Steve Maire, Jean Ernesta na Jean Claude Labrossa wote kutoka Shelisheli ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Kamishna ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda. Waamuzi watawasili nchini kesho (Aprili 18 mwaka huu) jioni.

MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI
Ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao uko nchini kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakutana na waandishi wa habari leo (Aprili 17 mwaka huu) saa 10 jioni hoteli ya Serena.

Mkuu wa Idara ya Uanachama ya FIFA, Primo Covarro ndiye aliyeongoza ujumbe huo ambao una siku tatu tangu ulipowasili nchini kushughulikia suala hilo.

Ujumbe huo jana (Aprili 16 mwaka huu) ulikutana na Sekretarieti ya TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, wagombea ambao walikata rufani FIFA na ambao waliomba marejeo (review) ya rufani zao kwa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF.

Leo asubuhi ujumbe huo wa FIFA ulitarajiwa kukutana na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Idd Mtiginjola.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment